You are currently viewing Vijana watakiwa kuchangamkia fursa sekta ya nishati
Screenshot

Vijana watakiwa kuchangamkia fursa sekta ya nishati

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Vijana wametakiwa kuchangamkia fursa zinazopatikana katika sekta ya nishati hapa nchini kwa kuwa sekta hiyo ina wigo mpana katika  kuzalisha ajira  kwa vijana sambamba na  kutoa mchango mkubwa katika kukuza pato la Taifa.

Hayo yamebainishwa jana Jumamosi na Mkurugenzi wa Idara ya Diplomasia na Uchumi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi John Ulanga kwenye kongamano la ‘nafasi ya vijana katika mapinduzi ya nishati barani Afrika’ lililoandaliwa na Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) katika chuo Kikuu cha UDOM jijini hapa.

Alisema sekta hiyo kwa sasa inahitaji vijana waliosoma ambao kwa sasa wanawakilisha  kundi kubwa katika jamii.

Alisema vyuo vingi  vikuu kwa sasa barani Afrika  pamoja na vile vya ufundi vinatoa mafunzo ya nishati jadilifu, uhandisi pamoja na uhifadhi wa mazingira na hivyo kuwataka  vijana kuchangamkia fursa hiyo, ili kuwa sehemu ya ukuaji wa uchumi na kujiongezea nafasi  katika soko la ajira pindi wanapohitimu.

Screenshot

“Kwa sasa  ajenda ya nishati jadilifu ni ajenda ya dunia,  endapo vijana watatumia vyema vyuo, makongamano na warsha katika kujiongezea maarifa watakuwa na nafasi ya kuajiriwa na uwezo wa kujiajiri ,hivyo kuwa  na mchango mkubwa katika kukuza pato la taifa,’’ alisema Balozi Ulanga.

Alitoa  mfano wa mpango wa Nishati Jadilifu barani Afrika (ARE) na ule wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB)  wenye kauli mbiu ya  ‘Ajira kwa Vijana barani Afrika’ambayo kwa pamoja yana malengo ya kuwawezesha vijana kitaaluma ili kuwa waendeshaji wakuu wa sekta hiyo.

“Naupongeza  mradi wa EACOP kwa kuendesha mafunzo mbalimbali yanayohusu sekta ya nishati kwa vijana  wa vyuo vikuu na Ufundi Stadi hapa nchini,,”

Screenshot

“Nina imani kuwa mijadala mbalimbali inayoibuka kwenye warsha  na mikutano  itasaidia kuongeza  hamasa ya vijana kushiriki  katika  sekta hii kikamilifu na hivyo kutoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi,’ alisema Balozi Ulanga.

Kwa upande wake  Mkurugenzi Mtendaji wa EACOP, Guillaume Dolout alisema  mradi huo wa kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Pwani ya Chongoleani mkoani Tanga umekuwa ukitoa mafunzo ya nishati kwa njia ya mtandao na vitendo kwa wanafunzi wa vyuo Vikuu na Ufundi katika nchi za Tanzania na Uganda.

“Kupitia mafunzo hayo, baadhi wa wahitimu wamekuwa wakipewa ajira katika maeneo mbalimbali ya mradi, huku wengine wakipata vyeti vitakavyo wawezesha  kujiajiri na kuajiriwa kupitia sekta hii popote duniani,’’ alisema Dolout.

Naye Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli hapa nchini (TPDC) linalomiliki hisa 15 kwa niaba ya Serikali katika mradi huo,  Derick Moshi alisema kuwa ushiriki wao katika kongamano hilo sio tu kama wahusika wa mradi wa EACOP, bali pia kuongeza hamasa kwa vijana kushiriki katika sekta ya nishati na gesi.

“Tumewapa elimu wanafunzi namna nishati na gesi kwa ujumla zinavyoendesha uchumi duniani, hasa katika nchi zinazoendelea, ili wao pia wajikite vizuri katika maeneo mbalimbali ikiwemo kufanya utafiti na ubunifu kupitia ukuaji wa tehama,” amesema.

Akizungumza kwa niaba wa wanahisa wakubwa katika mradi wa EACOP, TotalEnergies wanaomiliki asilimia 62, Mkurugenzi wa Sheria na Mahusiano, Bi. Getrude Mpangile amesema warsha hiyo ilikuwa  na lengo la kuwaelimisha vijana umuhimu wa sekta hiyo na fursa mbalimbali zinazopatikana.

“Tunapenda mradi huu uache wataalamu wa ndani wa kutosha pindi utakapokamilika na vijana wanaosoma katika vyuo vikuu na vya ufundi wana hiyo nafasi ya kushiriki katika ukuaji wa sekta hii hapa nchini,’’ alisema Bi. Mapangile.

Wanahisa wengine wa mradi wa EACOP ni Shirika la Mafuta nchini Uganda (UNOC) linalomiliki hisa asilimia 15 na Shirika la mafuta nchini China (CNOOC) linalomiliki hisa asilimia nane tu

Mmoja wa vijana waliopatiwa mafunzo katika Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), Nicolaus Shukuru anayesomea sekta ya Umeme Jadilifu alisema kupitia mafunzi hayo, wameweza kujifunza vitu mbalimbali, ikiwemo kubuni utaalamu katika shughuli zao utakao wasaidia kujipatia kipato.

Leave a Reply