You are currently viewing Viongozi wa dini: Marekani haiwezi kutugombanisha

Viongozi wa dini: Marekani haiwezi kutugombanisha

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT),  Sheikh Alhad Mussa Salum amesema jumuiya hiyo inapinga kauli ya maseneta wa Bunge la Marekani waliodai Tanzania si  salama na kuna udini huku baadhi ya wafuasia wa dini hizo hawatendewi haki.

Sheikh Alhad ameeleza kuwa yaliyosemwa na maseneta hao ni uzushi na jambo ambalo halikubaliki na kauli zao zinalenga uchochezi wa wa wazi wazi katika Taifa.

Ametoa msimamo huo leo Mei 26,2026 Jumanne jijini Dodoma wakati wa mkutano wa wanahabari na JMAT.

JMAT ni jumuiya inayounganisha au yenye mjumuiko wa madhehebu mbalimbali ya dini za Kiislamu, Kikristo na nyingine.

” Uwepo wetu leo hapa ni kielelezo tosha kwamba hakuna udini Tanzania, Tunaitaka Serikali ya Marekani iwakemee maseneta mara moja na ikanushe kauli waziwazi kwamba kwamba kauli hiyo itabaki kuwa kauli yao binafsi,”

“Kwetu sisi Watanzania imetuumiza sana kwa sababu, umoja na mapenzi tulionayo kama Watanzania ni makubwa na kielelezo cha viongozi tulio hapa mbele cha undugu wa damu baina ya Waislam na Wakristo,”

Amesema viongozi wa dini wa Tanzania, wana ushirikiano na undugu wa damu hivyo maseneta wa Marekani wamechelewa kwa hatua ya kutaka kuwachonganisha.

” Wamechelewa ni jambo ambalo haliwekezani, tunaomba waendelee kuiheshimu Tanzania ambayo inatawaliwa kwa misingi ya sheria, kanuni na Katiba.Waendelee kuheshimu mamlaka, uchochezi wa kidini au siasa hatutaukubali kama Watanzania,” amesema Sheikh Alhad.

Amesema Watanzania wanaungana viongozi wa dini na Serikali kupinga udini, siasa chafu na uchonganishi.