Ndege zisizopungua 10 za mashirika tofauti ya ndege nchini India, zimelazimika kusitisha safari zake za ndege, kuchelewesha ratiba na kubadili njia za safari zake baada ya kupokea vitisho vya mabomu ndani ya saa 48 zilizopita.
Hali hiyo inatajwa kuwa jambo la kawaida kwa mashirika ya ndege nchini India kupokea vitisho vya mabomu lakini kuanzia Jumatatu ya wiki hii, vitisho vimeongezeka na kuzua taharuki katika ndege hizo zinafanya safari kuelekea maeneo mbalimbali duniani.
Juzi Jumanne, Jeshi la Anga la Singapore lilituma ndege mbili za kivita kuisindikiza ndege ya Air India Express, mbali na maeneo yenye watu wengi kufuatia tishio la bomu, huku saa chache kabla ya hapo, ndege ya Air India kutoka Delhi kwenda Chicago ikilazimika kutua katika Uwanja wa Ndege wa Canada kama hatua ya tahadhari.
Awali, Jumatatu, ndege tatu za kimataifa zilizokuwa zimeondoka Mumbai, zililazimika kucheleweshwa baada ya akaunti ya X (Twitter) kuchapisha vitisho ambapo polisi wamemkamata kijana mmoja kuhusiana na tukio hilo.
Lakini pia Jumanne, ndege saba, zikiwemo mbili za Air India, ziliathiriwa na vitisho vilivyotolewa na akaunti nyingine ya X ambayo sasa imezuiliwa. Picha za skrini za baadhi ya machapisho zinaonyesha mtumiaji alikuwa ametaja shirika la ndege na polisi wa eneo husika na kutaja namba ya ndege.
Air India ilisema katika taarifa kwamba ilikuwa inashirikiana na mamlaka kutambua watu waliohusika na vitisho hivyo na ingefikiria kuchukua hatua za kisheria ili kufidia hasara iliyopatikana. Kila Uwanja wa Ndege nchini India una Kamati ya Tathmini ya Vitisho vya Bomu ambayo inatathmini uzito wa tishio na kuchukua hatua ipasavyo, huku abiria hushushwa kutoka kwenye ndege pamoja na mizigo ya ndani ya ‘cabin’, na mizigo mingine, na yote hukaguliwa tena kuhakikisha usalama huku timu za uhandisi na usalama pia huchunguza ndege kabla ya kuruhusiwa kuruka tena