You are currently viewing Vitongoji 89 Magu kufikiwa na umeme 2028

Vitongoji 89 Magu kufikiwa na umeme 2028

JUMLA ya vitongoji 89 vilivyopo katika vijiji vya kata mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya ya Magu, mkoani Mwanza vinatarajiwa kufikiwa na huduma ya umeme ifikapo Disemba mwaka 2028.

Hayo yameelezwa jana Jumatano na Msimamizi wa miradi ya umeme wilayani Magu, Ibrahim Msafiri kwa niaba ya Meneja wa TANESCO wa wilaya hiyo, wakati akijibu maswali ya madiwani kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo.

Katika swali hilo ambalo liliongezewa msisitizo na Diwani wa kata ya Kahangara, Daudi Makologoto, alihoji ni lini zoezi la uwekaji nguzo kwenye vitongoji 89 linatakamilika wakati Magu ina vitongoji 508.

Akijibu swali hilo, Msafiri alisema; “Zoezi la ufikishaji wa huduma ya umeme katika vitongoji 89 litakamilika Disemba mwaka 2028. Hivi sasa mkandarasi ana mkataba wa miaka mitatu kuanzia Januari 2026 ambapo zoezi la upimaji limekamilika, sasa anakusanya vifaa kuelekea ‘site’.

“Kwa kuwa mkataba wake unatarajiwa kuisha Disemba mwaka 2028, niwahakikishie waheshimiwa madiwani, vitongoji hivyo vitakuwa vimefikiwa na umeme,” amesema.

Naye Diwani wa kata ya Nyanguge, Hilali Elisha alihoji kwanini Tanesco inatoza wananchi gharama za uunganishwaji umeme pamoja na ankara ya huduma yake kiwango cha miundo ya miji ilihali halmashauri hiyo miundo yake bado ni vijiji.

“Serikali kupitia wizara ya nishati imekuwa ikisisitiza vijiji visivyokuwa na miundo ya miji viunganishiwe umeme kwa gharama ya Sh 27,000. Je, lini utekelezaji wake utaanza kwa sababu wananchi wengine hawajapata umeme kwa sababu wameshindwa kumudu gharama ya Sh 321,000 ya kuunganishiwa umeme?.

Aidha, akijibu swali hilo, Mkuu wa wilaya ya Magu, Jubilate Lawuo alisema suala hilo la Tanesco kutoza gharama kubwa kwa vijiji sawa na miji, limeshafika mezani kwake na amemuandikia barua mkurugenzi mkuu wa Tanesco, hivyo mchakato wa kurejesha ankara na usambazaji umeme kwa kuzingatia mfumo wa vijiji unaendelea.