WADAU wa sanaa katika Halmashauri ya Wilaya ya Magu mkoani Mwanza wametakiwa kujisajili katika Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ili watambulike kitaifa na kupata manufaa katika fursa mbalimbali zinazojitokeza kwenye sekta hiyo.

Wito huo umetolewa leo Jumatano tarehe 7 Mei, 2025 na Mkuu wa Kitengo cha Utamaduni, Sanaa na Michezo, Peter Mujaya alipokutana na wadau hao katika mafunzo ya siku moja yaliyofanyika kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo zilizopo Ilungu.
Akifafanua kuhusu malengo ya mafunzo hayo, Mjaya amesema pamoja na mambo mengine, mafunzo hayo yalilenga kuwaeleza wadau hao wa sanaa namna ya kuinua kiwango cha sanaa Magu na kuwaeleza manufaa ya mfuko wa mikopo ya shughuli za utamaduni inayotolewa na Serikali kwa wasanii.

“Ili uweze kupata mikopo hii kwanza lazima uwe umejisajili BASATA, lakini pia kiwango cha mkopo kinategemea na malengo yako kwamba unahitaji mkopo kwenda kufanyia nini, labda kununua vifaa vya muziki wa aina Fulani au lah,” amesema.
Ameongeza kuwa mikopo hiyo inalenga kuwajengea uwezo wadau hao wa sanaa katika shughuli za sanaa na utamaduni
“Lakini pia katika mafunzo haya tumefanikiwa kuunda umoja wa wasanii Magu ambao unajumuisha wale wote wanaojishughulisha na shughuli zote za Sanaa,” amesema.
Wakizungumzia mafunzo hayo, baadhi ya wadau hao wa sanaa Amos Saulo ameishukuru halmashauri ya Magu kwa kuwaandalia mafunzo hayo ambayo yamewafungulia njia kwa kutambua mambo mbalimbali ambayo yalikuwa na faida kwao.
“Kwa kweli tunashukuru sana kwa mafunzo haya kwa sababu hata mimi binafsi nilikuwa nakwepa kujisajili nikidhani nitajiongezea mzigo wa kodi kutoka TRA, ila sasa nitakwenda kujisajili kwa sababu nimegundua ninajikosesha fursa muhimu za kukua kisanaa,” amesema.
Mafunzo hayo yamehudhuriwa na wanamuziki wa aina mbalimbali, wazalishaji video za muziki, washerehesaji ‘Mc’s’ na kampuni zinazofanya shughuli za sanaa ikiwamo kutangaza na kukodisha muziki kwenye sherehe na matukio mbalimbali.