Mamlaka nchini Ugiriki zimesema wahamiaji zaidi ya 500 wameokolewa kwenye kisiwa cha kusini mwa nchi hiyo cha Crete, mojawapo ya malango yanayotumiwa na watu wanaotaka kuingia Ulaya kimagendo wakitokea Asia na Afrika.
Miongoni mwa waliookolewa ni wahamiaji 280 katika misafara mitano tafauti, ambao ndani yake walikuwamo watoto 13, kwa mujibu wa walinzi wa pwani wa Ugiriki.
Kisiwa cha Crete kinachotazamana na Libya na Misri kimekuwa kikipokea idadi kubwa ya wahamiaji katika miaka ya hivi karibuni.
Wahamiaji hao hutumia njia za hatari na mashua zisizo salama kuvuukia, ambapo miaka miwili iliyopita meli iliyosheheni watu kwenye ujia wa kusini magharibi wa Peloponnese ilizama na kuuwa watu zaidi ya 600 waliokuwamo, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.