You are currently viewing Wananchi Mwamanga waishukuru serikali kuwapatia hatimiliki za kimila

Wananchi Mwamanga waishukuru serikali kuwapatia hatimiliki za kimila

Wananchi wa Kijiji cha Mwamanga, Kata ya Mwamanga wilayani Magu wameishukuru serikali kwa kuwapimia maeneo yao na kuwapatia hati za hakimiliki za kimila hatua inayoelezwa kuwa itapunguza migogoro na kupandisha thamani ya ardhi zao.

Shukrani hizo wamezitoa wakati wa zoezi la ugawaji wa hati kwa wananchi wa Kijiji hicho ambapo hati 868 zilitolewa mara baada ya serikali kupitia wizara ardhi na halmashauri ya wilaya ya Magu  kuendesha zoezi la kufanyika mpango wa matumizi bora ya ardhi  pamoja na upimaji wa ardhi katika Kijiji hicho.

Akizungumza baada ya kupokea hati zake, Bi. Yunis Lubeja mkazi wa Mwamanga ameishukuru serikali kwa hatua hiyo na kubainisha  kuwa upatikanaji wa hati za ardhi utawasaidia kuongeza thamani ya ardhi zao pamoja na kupunguza migogoro ya ardhi iliyokuwa ikiibuka mara kwa mara.

Alibainisha kuwa wakati Serikali ilipoanza zoezi la kupanga na kupima maeneo, baadhi ya wananchi walidhani ni utapeli na walihofia kuporwa ardhi zao. Hata hivyo, baada ya kuona matokeo chanya ya zoezi hilo, aliishukuru Serikali kwa ufanisi wake na kuwasihi wananchi wengine ambao bado hawajapimiwa maeneo yao kujitokeza ili nao wanufaike na mpango huo.

Kwa upande wake, Afisa Ardhi wa Halmashauri ya wilaya ya Magu Bw. Gracian Nyangindu aliwashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi hilo na kuwataka kuzitunza hati zao vizuri.

 Alisisitiza umuhimu wa hati hizo kama nyaraka halali za umiliki wa ardhi na kuwaasa wananchi kuzitumia kwa maendeleo yao na ya kijiji kwa ujumla.

Leave a Reply