Watu wa jamii zinazoishi pembezoni mwa miji wanaojulikana kama watu wa asili wameupongeza mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kwa kuendelea kuheshimu mila, tamaduni na desturi zao wakati wa utekelezaji wa mradi huu.
Pia wamepongeza mradi huo kwa kuendelea kuwashirikisha katika kila hatua ya utekelezaji kupitia mikutano inayofanyika mara moja kila baada ya miezi mitatu kwa mwaka, ili kupewa taarifa za maendeleo ya mradi na kujadiliana kwa pamoja juu ya fursa au changamoto yoyote inayoweza kujitokeza katika maeneo yao wakati mradi huu unaendelea kutekelezwa.
Monica Kilandi, ambaye ni kiongozi wa kimila kutoka kabila la Kimasai amesema wakiwa kama sehemu ya waguswa, tamaduni, mila na desturi zao zimeendelea kuheshimiwa na hilo ni jambo la kujivunia.
“Hatukupata athari yoyote walipokuja katika maeneo yetu zaidi ya sisi kufaidika kwa kujengewa uwezo na kuboreshewa huduma za kijamii.
“Kwa mfano, tuna changamoto ya maji katika maeneo yetu yanayoathiriwa na ukame na mradi tayari umeahidi kutusaidia.
“Lakini pia mradi unatujengea uwezo akina mama wa kimasai wa kusikilizwa mahitaji yetu muhimu katika kijamii kwa sababu kutokana na tamaduni zetu ni vigumu kuongea mambo yanayotuhusu mbele ya wanaume, lakini mradi wa EACOP umekuwa ukiitisha vikao vya akina mama wa kimasai na kujadili mambo yanayotugusa,” amesema.
Naye Naseliani Lembulisi Remama wa Kiteto anayewakilisha jamii ya Wa-akie anasema tamaduni zao, ikiwemo maeneo yao ya kuabudu yamekuwa yakiheshimiwa kwa sababu mradi kabla ya kufanya jambo lolote linawashirikisha wakuu wao wa kimila kwanza na kuja na maamuzi ya pamoja.
“Tunaushukuru mradi na sasa kwa kuheshimu mila, tamaduni na desturi na sisi Kabila la Wa-kie tumeuomba mradi wa EACOP kutusaidia kupata hati ya umiliki wa kimila ya eneo letu la kufanya ibada, upimaji tayari umefanyika tayari na sasa tunasubiri tu hati ya eneo hilo.
“Kwa dhati kabisa ushirikishwaji wetu katika mradi huu umekuwa na faraja sana na sisi kama watu wa pembezoni na ujio wa mradi huu umetupa faida mbalimbali ikiwemo vijana wetu kupata ajira,” amesema
Mmoja wa viongozi wa kimila kutoka jamii za Wataturu mzee Shingalila Kishaida Mniri kutoka wilaya ya Igunga anasema mradi uliathiri maeneo ya jamii ya watu wake wa pembeni na walilipwa fidia nzuri sana iliyobadili kabisa maisha yao.
Lakini pia amesema mradi umeheshimu tamaduni yao ambapo ulikubali kuchepusha njia ya bomba la mafuta katika maeneo yao ya makaburi ambayo kwa tamaduni zao hayatakiwi tena kufukuliwa.
“Tulipowaambia watu wa mradi wa EACOP kuhusu jambo hili, waliheshimu mila hiyo na badala yake walishepusha njia ya bomba na makaburi yetu kubaki salama,” amesema.
Kwa mujibu wa Dk. Elifuraha Laltaika ambaye ni Mshauri wa mradi wa EACOP kwa watu waguswa wanaoishi pembezoni mwa mji, mradi huu umekuwa ukikutana na jamii hizo mara moja kila baada ya miezi mitatu kujadili maendeleo ya mradi na kuangalia maeneo ambayo wanaweza kushirikiana.
Amesema mradi huu unaheshimu mila na tamaduni kwa kufuata sheria za nchi na za kimataifa ambapo mradi huu umeridhia sera za kimataifa za haki za binadamu na kuheshimu makundi ya jamii za Masai, Wa-akie, Wa-Bargaig pamoja na Wataturu.
Mradi wa EACOP ambao unapita katika mikoa nane hapa nchini, una urefu wa kilomita 1,443 kutoka Hoima nchini Uganda hadi rasi ya Chongoleani mkoani Tanga.
Wanahisa ni TotalEnergies yenye asilimia 62, wakati Mashirika ya Maendeleo ya mafuta (TPDC- Tanzania na (UPDC kwa upande wa Uganda) yana miliki asilimia 15 kila moja na shirika la mafuta la China (CNOOC) linamiliki asilimia nane tu katika mradi huu.