Watuhumiwa watano akiwamo katibu wa Mbunge wa Kilolo, Kefa Walles, Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi kupitia CCM wilaya ya Kilolo, Hedikosi Kimwaga, Diwani kata ya Nyanzwa, Boniface Ugwale maarufu kama ‘Katili’, Wille Chikweo na Silla Kimwaga wamefikishwa mbele ya Mahakama ya wilaya ya Iringa kwa tuhuma za kumuua aliyekuwa katibu wa CCM Wilaya ya Kilolo, Christina Kibiki.
Kesi hiyo ya Jinai namba 34404 ya mwaka 2024 iliyowahusisha baadhi ya viongozi wa CCM imesomwa mbele ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Iringa, Rehema Mayagilo na kusimamiwa na mwendesha mashtaka upande wa Jamhuri Sauli Makori.
Imeelezwa mahakamani hapo kuwa watuhumiwa hao walitenda kosa hilo Novemba 12, 2024 eneo Banawanu lililopo kata ya Mseke majira ya usiku nyumbani alipokuwa akiishi Marehemu Christina Kibiki.
Hata hivyo, watuhumiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwani upelekezi wa kesi hii bado unaendelea hivyo kesi imeahirishwa hadi Januari 7, 2025 ambapo itakuja tena kwa ajili ya kutajwa.
Ikumbukwe Christina Kibiki aliuawa kikatili kwa kuchomwa na vitu vyenye ncha kali eneo la tumboni kisha kupigwa risasi na watu wasiojulikana usiku wa novemba 12, 2024 akiwa nyumbani kwake.
Watuhumiwa wote wamerudishwa rumande wakisubiri tarehe tajwa kwaajili kujibu kesi inayowakabili baada ya upelekezi wote kukamilika.