You are currently viewing Waziri ahukumiwa kifo kwa ubadhirifu

Waziri ahukumiwa kifo kwa ubadhirifu

MAHAKAMA ya Watu ya Kati katika mji wa Changchun, Mkoa wa Jilin, imemhukumu Waziri wa zamani wa Kilimo na Masuala ya Vijijini wa China, Tang Renjian, adhabu ya kifo itakayositishwa kwa miaka miwili, baada ya kupatikana na hatia ya kupokea hongo ya takribani dola milioni 38 sawa na Sh bilioni 92.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Xinhua, Tang pia amepokwa haki zake zote za kisiasa milele, huku mali zake binafsi zikitaifishwa na fedha alizopata kwa njia haramu zikikabidhiwa kwa serikali.

Mahakama ilibaini kuwa kati ya mwaka 2007 na 2024, Tang alitumia nyadhifa zake za juu katika ngazi za kitaifa na mitaa kusaidia watu wengine kupata mikataba ya biashara, kushinda zabuni za miradi na kupandishwa vyeo, na kwa malipo alipokea hongo hizo.

Majaji walihitimisha kuwa makosa hayo yalisababisha madhara makubwa kwa maslahi ya kitaifa na ya umma, na hivyo kustahili adhabu ya kifo. Hata hivyo, mahakama ilionyesha huruma kwa sababu Tang alishirikiana na wachunguzi, alikiri makosa, alirudisha mali zilizopatikana kwa njia haramu, na kuonyesha majuto.

Leave a Reply