Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amekutana na Mfalme Charles III wa Uingereza, pembezoni mwa Mkutano wa Viongozi wa Jumuiya ya Madola (CHOGM 2026) unaofanyika Kisiwani Antigua, nchini Antigua na Barbuda.
Katika mkutano huo, Balozi Kombo akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, pia alikutana na Waziri Mkuu wa Uingereza, Andy Burnham, Waziri Mkuu wa Antigua na Barbuda, Gaston Browne, pamoja na Gavana Jenerali wa Antigua na Barbuda, Sir Rodney Williams.
Mkutano wa CHOGM unawakutanisha viongozi wa Serikali za nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola pamoja na wadau wa sekta binafsi kwa lengo la kujadili fursa za uwekezaji, kuimarisha ustahimilivu wa uchumi na kukuza ajira katika nchi wanachama.
Majadiliano katika mkutano huo yalijikita katika maeneo ya miundombinu, nishati jadidifu, kilimo na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, huku yakisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa vitendo kati ya Serikali na wawekezaji pamoja na kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika maendeleo ya nchi wanachama.
Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo ni fursa muhimu ya kuimarisha mahusiano ya kimataifa na kuendeleza diplomasia ya uchumi kwa lengo la kuvutia uwekezaji, kukuza ustawi wa pamoja na kuendeleza ushirikishwaji wa sekta binafsi katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
