You are currently viewing Waziri mkuu kuzindua meli mpya MV. New Mwanza

Waziri mkuu kuzindua meli mpya MV. New Mwanza

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (MB) anatarajiwa kuzindua Meli ya kisasa ya MV New Mwanza katika Bandari ya Mwanza Kusini kesho ijumaa tarehe 23 Januari, 2026.

Hayo yamebainishwa na Mhe. Prof. Makame Mbarawa (MB), Waziri wa Uchukuzi leo tarehe 22 Januari, 2026 wakati akizungumza na Waandishi wa Habari katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.

Prof. Mbarawa amesema Meli ya MV Mwanza imejengwa na Mkandarasi Gas Entec Ship- Building kutoka Korea kwa kushirikiana na Kampuni ya Meli nchini (TASHICO) kwa gharama ya Tshs. Bilioni 120.56 huku akieleza kuwa Ujenzi wa Meli hiyo umezingatia teknolojia za kisasa na mpaka sasa meli hiyo imefanyiwa safari sita za majaribio (Mwanza – Bukoba) kuanzia mwezi Machi 2025 ambapo yameonesha ufanisi mkubwa na TASAC.

Aidha, ameongeza kuwa Meli hiyo ya ghorofa 4 ndiyo kubwa zaidi ya zote ndani ya ukanda wa maziwa makuu na ina uwezo wa kubeba abiria 1200, tani 400 za mizigo, magari madogo 20 pamoja na makubwa 3 kwa wakati mmoja.

Pia Waziri Mbarawa amesema kuwa kabla ya Uzinduzi huo Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atafanya ziara ya kikazi katika Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Kuratibu Shughuli za Utafutaji na Uokoaji (MLVMCT) kilichopo Wilaya ya Ilemela eneo la Uwanja wa ndege hapa Mkoani Mwanza.

Lengo la ziara hiyo ni kukagua na kujionea hatua ya ujenzi wa Kituo hicho ikiwa ni pamoja na maandalizi, mifumo ya uratibu, na kuona uwezo wa kitaalamu uliopo katika kukabiliana na matukio ya dharura yanayohusisha utafutaji na uokoaji, hususan katika maeneo ya Ziwa Victoria na maeneo jirani na namna kitakavyofanya kazi.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ametumia wasaa huo kuwakaribisha wananchi wa Mkoa huo pamoja na mikoa ya jirani kumlaki na kushiriki kwenye ziara hiyo ya kitaifa ya Mhe. Waziri Mkuu kuanzia saa 2 asubuhi.

Leave a Reply