Serikali kupitia Wizara ya Afya, imesema dawa za kufubaza makali ya Virusi vya UKIMWI (ARVs) haziuzwi na kwamba zipo za kutosha.
Imeongeza kuwa watumiaji wa dawa hizi, hawana sababu ya kuwa na wasiwasi kuhusu upatikanaji wa dawa hizi.

Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Afya, Roida Andusamile imesema Serikali kupitia Wizara inaendelea kuweka mikakati thabiti na stahiki ili kuhakikisha huduma zinaendelea kutolewa kama kawaida.
Aidha, Wizara imetoa rai kwa wananchi kupuuza taarifa hizi na kuendelea kutumia dawa kwa usahihi kama wanavyoelekezwa na wataalam wa afya ili kuzuia usugu wa vimelea vya magonjwa haya dhidi ya dawa.
Taarifa ya Wizara ya Afya imekuja baada ya uwepo wa taarifa kwenye mitandao ya kijami pamoja na vyombo vingine vya habari zikielezea uhaba wa dawa za kufubaza makali ya Virusi vya UKIMWI (ARV), na kwamba sasa watumiaji wanalazimika kununua dawa hizo.
Taarifa hiyo imesema huo ni upotoshaji na taarifa hizo zimeleta hofu miongoni mwa wananchi na kusababisha baadhi ya wagonjwa kuomba kupewa dawa za muda mrefu kwa ajili ya akiba, jambo ambalo si sahihi na linaweza kuathiri utunzaji na matumizi sahihi ya dawa.