You are currently viewing WorldVeg, AID-I watoa mafunzo kwa wakulima 62,000 
Screenshot

WorldVeg, AID-I watoa mafunzo kwa wakulima 62,000 

Na Mwandishi Wetu, Arusha

Zaidi ya wakulima 62,000 wadogo wadogo nchini wamenufaika na mafunzo ya kilimo cha mbogamboga na matunda yaliyotolewa na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti na Uendelezaji wa Kilimo cha Mbogamboga – Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (World Vegetable Center – WorldVeg) ili kuwasaidia kuongeza uzalishaji na kujikwamua kiuchumi.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa hafla ya kufunga rasmi utekelezaji wa mradi huo unaoitwa Accelerated Innovation Delivery Initiative (AID-I), wenye kauli mbiu isemayo “Kusherehekea ushirikiano, matokeo, na ubunifu katika mifumo ya mbegu, minyororo ya thamani, na lishe”, Meneja wa Programu wa WorldVeg – Tanzania, Bi. Colleta Ndunguru, alisema mradi huo umekuwa na tija toka kuazishwa kwake mwaka 2023 katika mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro pamoja na visiwani Zanzibar.

Meneja wa Programu Tanzania  wa Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti na Uendelezaji wa Kilimo cha Mbogamboga Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (World Vegetable center),  Bi. Colleta Ndunguru (katikati) akikabidhi  cheti kwa wanufaika wa mradi wa ‘Accelerated Innovation Delivery initiative’ (AID-I)  kwa upande wa   Zanzibar wakati wa hafla  fupi ya kufungwa kwa mradi huo, liyofanyika kwenye taasisi ya WorldVeg iliyopo Tengeru mkoani Arusha jana. Kulia ni  Mratibu wa Nchi kutoka Taasisi ya Kimataifa ya  International Maize and Wheat |Improvement Center (CIMMYT), Bw. Peter Ojukwu, kushoto ni Bi. Maryam Salim na (wapili kushoto) ni Jeremiah Sigalla Meneja Mradi wa AID-I.

“Mradi huu umegusa maeneo mbalimbali ikiwemo kusaidia wakulima kurasimisha biashara zao ili zitambulike kisheria, sambamba na kusambaza mbegu bora za mbogamboga kwa zaidi ya kaya 10,500,” alisema Bi. Ndunguru.

Aliongeza kuwa zaidi ya wakulima 62,000 wamenufaika toka mradi huo unaofadhiliwa na Taasisi ya Kimataifa ya Uboreshaji wa Mahindi na Ngano (CIMMYT) uanzishwe hapa nchii, huku takriban wazalishaji wa mbegu 10,684 wakipatiwa mafunzo,  asilimia 52 kati yao wakiwa wanawake na asilimia 29 vijana.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo na Mifugo Zanzibar, Dkt. Abdallah Ibrahim Ali, aliipongeza WorldVeg kwa mchango huo mkubwa katika kuinua kilimo cha mbogamboga na matunda hapa nchini.

Screenshot

“Kupitia mradi huu, maelfu ya vijana wamenufaika , huku zaidi ya miche 446,021 ya mboga ikisambazwa katika mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar,” alisema Dkt. Ali.

Alisisitiza umuhimu wa kuendelezwa kwa mradi huu katika maeneo ambayo bado haijafikiwa ili kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wananufaikan na kuongeza tija ya kilimo katika uchumi wa taifa.

Naye Mratibu wa Nchi kutoka CIMMYT, Bw. Peter Ojukwu, alisema sekta ya kilimo inakabiliwa na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi, ambayo huathiri usalama wa chakula.

Amesema kuwa kutokana na changamoto hizo, CIMMYT ilimua kuanzisha mradi huo wa AID-I ili kukabiliana na tatizo la njaa na lishe duni kwa kutoa elimu na mafunzo bora juu ya uzalishaji wa mbegu na uongezaji thamani wa mazao, hasa mbogamboga na matunda.

Meneja wa Programu Tanzania  wa Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti na Uendelezaji wa Kilimo cha Mbogamboga Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (World Vegetable center),  Bi. Colleta Ndunguru. Akizungumza na wabia wa maendeleo  katika sekta ya kilimo cha mbogamboga na matunda pamoja na wanufaika wa mradi wa ‘Accelerated Innovation Delivery initiative’ (AID-I) hawapo pichani,  wakati wa hafla  fupi ya kufungwa kwa mradi huo, liyofanyika kwenye taasisi hiyo iliyopo Tengeru mkoani Arusha jana.  

“Tunaipongeza WorldVeg kwa kazi nzuri ya kuwaunganisha wadau wa sekta ya kilimo cha mbogamboga na matunda, jambo ambalo linasaidia kutambua changamoto na kuzigeuza kuwa fursa kwa wakulima wadogo,” alisema Bw. Ojukwu.

Mmoja wa wanufaika wa mradi huo, Bw. Michael Slaa kutoka Wilaya ya Karatu, alisema kupitia mradi huo wamepata uhakika wa soko na kipato.

“Awali tulikuwa tunazalisha gunia 40 za vitunguu kwa heka moja, lakini baada ya kupewa mafunzo haya, hivi sasa tunazalisha gunia kati ya 100 hadi 120 kwa heka,” alisema Bw. Slaa.

Naye Bi. Maryam Salim kutoka Wilaya ya Chake Chake – Pemba, alisema mradi huo umemuwezesha kupata kipato endelevu kwa kuzalisha mbegu za mchicha lishe na kuziuza kwa wakulima wenzake.

Mradi wa AID-I umewezeshwa na ushirikiano kati ya WorldVeg na mashirika washirika mbalimbali ikiwemo  RIKOLTO, IDP, World Vision, HollandGreentech, Kilimo Trust, SAIPRO, Froresta, Milele Zanzibar Foundation, na Wizara ya Utalii na Urithi – Zanzibar.

Leave a Reply