Tozo za viza za kuingia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa madereva wa malori wa Tanzania zitaendelea kulipwa na kwamba pande mbili zimehimizwa kuendelea na mazungumzo ya kuangalia namna ya kuondoa tozo hizo.
Kauli hiyo imetolewa jana Aprili 01, 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Uhamiaji ya DRC, Bw. Roland Kashantwale alipokutana na Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Said J Mshana na Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo nchini Tanzania, Jean Pierre Masalla kufafanua kuhusu tangazo ambalo DRC imelitoa la kufuta malipo ya viza kwa Watanzania wanaoingia nchini DRC.

Bw. Kashantwale amesema utaratibu uliotangazwa hautawanufaisha madereva wa Tanzania wanaoendesha magari ya mizigo kwa kuwa wao, wataendelea kutozwa malipo ya visa ya kazi (Work Transit Visa) ya Dola 50 kwa siku 30.
Bw. Kashantwale amesisitiza umuhimu wa nchi mbili kuendelea na mazungumzo ili kupata muafaka wa kuondoa malipo ya visa ya kazi (Work Transit Visa) ya Dola 50 na kabla muafaka huo haujafikiwa, malipo hayo yataendelea kulipwa kwa madereva wa malori wanaoingia DRC.