Chama cha National League for Democracy (NLD) kimemtangaza rasmi, mwanachama na Katibu Mkuu wao, Doyo Hassan Doyo, kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu.
Hatua hiyo imetokana na kukamilisha taratibu za mchakato wa ndani wa chama hicho na kuwapitisha rasmi wagombea wake wa nafasi za juu katika Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2025, akiwamo Doyo kama mgombea urais na Mfaume Khamis kuteuliwa kama mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama ya NLD.
Taarifa iliyotumwa kwenye vyombo vya habari na kitengo cha habari cha NLD, imesema uamuzi huo umetokana na vikao halali vya chama, kufuata taratibu zote za kikatiba, na mapendekezo ya wajumbe wa mkutano mkuu kutoka sehemu mbalimbali kote nchini.
“Tuna imani kubwa kwamba viongozi hawa ni mfano wa uongozi bora, wenye maono makubwa ya kuleta mabadiliko ya kweli kwa Watanzania wote. Chama cha NLD kimejizatiti kuendeleza misingi ya demokrasia, Uzalendo, haki, na maendeleo jumuishi kwa kila Mtanzania,”ilisema taarifa hiyo.
NLD kimekuwa chama cha pili kutangaza mgombea wake wa urais, baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kufanya hivyo mapema mwaka huu kwa kumtangaza Dkt. Samia Suluhu Hassan kama mgombea wao wa urais.