Kiutamaduni Mapapa huchaguliwa na makasisi wakuu wanaoitwa Makadinali kupitia mchakato wa uchaguzi wa siri ulioanzia karne nyingi nyuma.
Papa mpya huchaguliwa baada ya aliyemadarakani kufariki, au baada ya kujiuzulu kama Papa Benedict XVI alivyofanya, mwaka 2013.
Mrithi wake anakuwa kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki la Roma – Papa Mkuu.
Mwanaume yeyote Mkatoliki aliyebatizwa anaweza kuchaguliwa kuwa Papa. Hata hivyo, kazi hiyo huenda kwa mmoja wa maofisa wakuu katika Kanisa Katoliki, anayeitwa Kadinali. Pia makadinali ndio wanaomchagua Papa mpya.
Kuna makadinali 252 kote ulimwenguni kufikia tarehe 19 Februari 2025, ambao kwa kawaida pia ni maaskofu. Na wale walio chini ya umri wa miaka 80 ndio wanaostahili kumpigia kura papa mpya.

Idadi ya makadinali wanaopiga kura kwa kawaida hupunguzwa hadi 120, lakini kwa sasa kuna 138 kati yao ambao wana vigezo vya kushiriki katika kumchagua Papa mpya. (Papa Francis aliteua Makadinali wapya 21 mwezi Desemba 2024.)
Ukifika muda wa kumchagua Papa mpya, Makadinali wote wanaitwa Vatikani huko Roma kwa mkutano. Kwa ajili ya mchakato wa uchaguzi ambao umefanyika kwa karibu miaka 800.
Katika siku ya kwanza ya kongamano hilo, wanafanya Misa (ibada ya Kikristo) katika Kanisa la St Peter’s Basilica. Kisha wanakusanyika katika Kanisa la Sistine la Vatikani. Huko, agizo la “extra omnes” hutolewa. Ni lugha ya Kilatini ikiwa na maana “kila mmoja atoke nje.”
Kuanzia wakati huo, Makadinali wote watawekwa ndani ya Vatican hadi papa mpya atakapochaguliwa.
Makadinali wanaopiga kura wana chaguo la kuanza kupiga siku ya kwanza wakiwa Sistine Chapel. Kuanzia siku ya pili na kuendelea, hupiga kura mara mbili kila asubuhi, na mara mbili kila alasiri, hadi mgombeaji wa Upapa apatikane mmoja.
Katika kura hizo, kila Kadinali anayepiga kura huandika jina la mgombea anayempendelea kwenye karatasi za kupigia kura. Ili kuficha kura, Makadinali wanaambiwa wasitumie mtindo wao wa kawaida wa mwandiko.
Iwapo hakutakuwa na kura ya maamuzi kufikia mwisho wa siku ya pili, siku ya tatu hufanyika sala na tafakari, bila kupiga kura. Upigaji kura utaanza kama kawaida baada ya hapo.

Mgombea anahitaji theluthi mbili ya kura ili kuchaguliwa kuwa Papa.
Mchakato huo unaweza kuchukua siku kadhaa, au wakati mwingine wiki.
Mkutano huo hufanyika bila Makadinali kuondoka Vatikani, wala hawawezi kusikiliza redio, kutazama televisheni, kusoma magazeti au kuwasiliana na mtu yeyote hata kwa simu katika ulimwengu wa nje.
Hakuna mtu anayeruhusiwa kuingia katika makao ya Makadinali isipokuwa wahudumu wa nyumba, madaktari na makasisi wanaosikiliza maungamo yao. Wote hula viapo vya kutunza siri.
Kati ya muda mmoja wa kupiga kura na muda mwingine, Makadinali wote wapiga kura na wale ambao ni wazee sana wasioruhusiwa kupiga kura, hutumia muda huo kujadili sifa za wagombea.
Hakuna mtu anayeruhusiwa kufanya kampeni za wazi. Vatican inasema makadinali wanaongozwa na Roho Mtakatifu.
Mara mbili kila siku, karatasi za kupigia kura zilizotumika huchomwa moto. Na watu walio nje ya Vatikani wanaweza kuona moshi ukitoka kwenye bomba la kanisa la Sistine Chapel.
Rangi nyeusi au nyeupe huwekwa kwenye karatasi hizo. Moshi mweusi unaashiria bado hakuna matokeo; moshi mweupe unaonyesha kuwa Papa mpya amechaguliwa.
Mara baada ya Papa kushinda kura, papa mpya anaulizwa: “Je, unakubali kuchaguliwa kwako kama Papa Mkuu?”
Anachagua jina ambalo anataka litumiwe kuitwa kama Papa. Kisha Makadinali wanampa heshima na kuahidi utii wao.
Tangazo linatolewa kwenye roshani ya jengo la St Peter’s Basilica kwa umati uliopo chini. Tangazo hilo husema, “habemus papam”, ikiwa na maana: “Tumepata Papa.”
Jina la Papa mpya linafichuliwa, na Papa mwenyewe anaonekana. Anatoa kauli fupi na kutoa baraka za “urbi et orbi” – ikiwa na maana kwa “mji na ulimwengu.”
Baadaye, matokeo ya kila duru ya upigaji kura katika mkutano huo hupelekwa kwa Papa. Kisha hutiwa muhuri na kuwekwa katika hifadhi ya kumbukumbu ya Vatikani, na yanaweza kufunguliwa tu kwa amri ya Papa.