You are currently viewing Polisi yawatia mbaroni 8 wanaodaiwa kumteka Tarimo

Polisi yawatia mbaroni 8 wanaodaiwa kumteka Tarimo

HATIMAYE Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewakamata watuhumiwa nane wanaodaiwa kutaka kumteka Deogratius Tarimo, mkazi wa Kiluvya jijini Dar es Salaam.

Hatua hiyo imekuja ikiwa zimepita siku 23 tangu ‘clip’ za video zisambae katika mitandao ya kijamii zikionesha Tarimo akipambana na watuhumiwa hao waliotaka kumteka.

Taarifa ya kushikiliwa kwa watu hao imetolewa leo Jumatano tarehe 4 Disemba 2024 na Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Jumanne Muliro.

Katika taarifa yake amesema “tarehe 11 Novemba, 2024 eneo la Kiluvya Ubungo Dar es Salaam lilitokea tukio la kutekwa kwa Deogratius Tarimo, mfanyabiashara na mkazi wa Kibaha Mkoa wa Pwani.

“Kufuatia tukio hilo na mengine ya nyuma Polisi Dar es salaam imekuwa ikiendelea kuchunguza na kufuatilia taarifa mbalimbali pia kukusanya ushahidi wa kisheria kuhusiana na matukio hayo ili kuyazuia,” amesema.

Amesema Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam imefanikiwa kukamata kundi la wahalifu wanane wanaotuhumiwa kula njama kwa pamoja na baadae kufanya tukio la kumteka Deogratius Tarimo.

Amesema watuhumiwa hao wamekamatwa kwa nyakati tofauti Dar es salaam, Songea- Ruvuma na eneo la Mbingu Mlimba mkoani Morogoro.

“Pia lilipatikana gari aina ya Toyota Raum ambayo ilitumiwa wakati wa tukio hilo huku ikitumia namba isiyo halisi T 237 EGE na baada ufuatiliaji namba halisi ya gari hiyo ni T237 ECF.

“Watuhumiwa hao ni Bato Bahati Tweve (32) ambaye ni bondia, Miaka 32, Mkazi wa Kimara Bunyokwa na Songwe

Mbozi, Yusuph Abdallah (32), Mkazi wa Mbingu – Mlimba Morogoro, Fredrick Juma (31), Mkazi wa Kibamba na Nelson Elimusa (24) maarufu msela – dereva Tax, Mkazi wa Mbezi Luguruni.

“Wengine ni Benk Daniel Mwakalebela (40) maarufu tall, mkazi wa Mbezi -Makabe na Kyela Ipinda, Rusungo Mbeya, Thomas Ephraim Mwakagile (45) maarufu Baba Mage, mkazi wa Bunyokwa na Kyela Ngonga Ndiali- Mbeya, Anitha Alfred Temba (27), mkazi wa Mbezi Mwisho na Isack Mwaifani, maarufu boxer, mkazi wa Kimara Tembo Salanga na Bujonde Isanga Kyela, Mbeya,” amesema.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linaendelea na kazi ya kuzuia vitendo vya kihalifu pamoja na kuwakamata wote wanaojihusisha na matukio ya uhalifu.

Leave a Reply