KADA maarufu wa Chama Cha Mapinduz (CCM), Humphrey Polepole amejiuzulu Uongozi wa Umma akiwa kama Balozi na Mkuu wa Kituo cha Uwakilishi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Havana – Cuba, pamoja na Uwakilishi wa eneo la Karibe, Amerika ya Kati na nchi rafiki za Colombia, Venezuela na Guyana.
Katika barua yake aliyoiandika kwenda kwa Rais Samia Suluhu Hassan na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Polepole amedai kukosa imani na uongozi uliopo madarakani.
Katika barua hiyo aliyoiweka kwenye akaunti zake rasmi za mitandao ya kijamii, ina kichwa cha habari kinachesema – YAH: TAARIFA YA KUJIUZULU NAFASI YA UBALOZI NA NAFASI YA UONGOZI WANGU WA UMMA
Mheshimiwa Rais, Kwa heshima na unyenyekevu, naomba kukutaarifu kuwa nimefikia uamuzi wa kujiuzulu nafasi yangu ya Uongozi wa Umma nikiwa Balozi na Mkuu wa Kituo cha Uwakilishi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Havana – Cuba, pamoja na Uwakilishi wa eneo la Karibe, Amerika ya Kati na nchi rafiki za Colombia, Venezuela na Guyana.

Uamuzi huu si mwepesi, bali umetokana na tafakari ya kina juu ya mwenendo wa Uongozi katika nchi yetu, uzoefu wangu kama Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Novemba 2020 – Machi 2022), na hatimaye kama Balozi katika vituo vya Lilongwe- Malawi (Machi 2022 – Apili 2023) na Havana – Cuba (Aprili 2023- Julai 2025).
Mheshimiwa Rais, nilipokea kwa heshima kubwa uteuzi na dhamana uliyonipa kuwa mwakilishi wa nchi yetu katika ngazi ya kimataifa. Niliamini na ninaendelea kuamini lilikuwepo kusudi na kazi muhimu ya kuyashika, kuyasimika, kuyasimamia, kuyaimarisha na kuyaendeleza maslahi mapana ya nchi yetu katika maeneo ya uwakilishi ulinipa dhamana ya kuyasimamia.

Ni heshima kubwa na isiyopimika kuaminiwa kuwa Mwakilishi wako, Nchi yetu, Taifa letu, wananchi na Mamlaka ya nchi. Kwa hili, nasema asante.
Hata hivyo, kwa muda wote wa kuhudumu ndani na nje ya nchi, nimefuatilia kwa karibu na kushuhudia kwa masikitiko makubwa mwelekeo wa uongozi usiojielekeza ipasavyo katika kusimamia Haki za watu, Amani na kuheshimu watu, kufifia kwa dhamira ya kweli na uwajibikaji wa dhati wa kushughulikia kero na changamoto zao, na kudidimia kwa maadili ya uongozi katika ngazi mbalimbali.
Kudhoofika kwa utekelezaji wa majukumu ya msingi ya serikali kwa ajili ya ustawi wa wananchi; mambo haya yanateteresha maslahi rmapana ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Haya yote yamezidi kunifanya nikose amani ya moyo na imani katika uongozi niliopo ndani yake sasa.
Matukio ya hivi karibuni ya wazi ya kukiuka misingi, utamaduni na desturi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) – hususan katika mchakato wa uteuzi wa wagombea ndani ya Chama ambao kwa kila awamu huwa msingi wa kukihuisha Chama na fursa ya kufanya Mageuzi ambayo kwa pamoja hukipa chama sura ng’aavu mbele ya umma kabla ya uchaguzi; desturi hii ya kufarya mageuzi ndani ya chama imekuwa nguzo muhimu ya ukubalifu na ushindi wa CCM mbele ya umma.
Imekuwepo kauli maarufu ya CCM isemayo “Chama kwanza mtu baadaye”, mwanzoni mwa mwaka huu, nilipoona kauli hii inafanyika vinginevyo, nimejiuliza mara kadhaa ni maslahi ya nani yanapiganiwa wakati huu, mtu, kikundi au Chama Taasisi?
Kwa kuwa siwezi kuendelea kuwa sehemu ya uongozi usiohamasika na utii wa misingi ya katiba ya nchi na chama, haki, maadili, utu na uwajibikaji kwa wananchi, nimeamua kwa hiari yangu kujiuzulu nafasi yangu ya uongozi na utendaji serikalini.
Nitaendelea kuwa mwana CCM wa kawaida, mzalendo na raia mwaminifu kwa Taifa na nchi yetu.
Ninamwamini Mungu wa Mbinguni na ninahamasika na tumaini kuu kwamba siku moja nchi yetu itaongozwa kwa misingi ya haki, maadili, usimamizi thabiti wa miiko na nidhamu ya uongozi, dhamira njema, siasa safi, uongozi bora na hofu ya Mungu.
Mheshimiwa Rais, nakushukuru kwa fursa uliyonipa, naamini historia itatoa tafsiri sahihi ya hatua hii.
Kwa heshima kubwa,
Humphrey Hesron Polepole
Nakala:
Katibu Mkuu
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dodoma