You are currently viewing Masista wanne wafariki dunia Mwanza

Masista wanne wafariki dunia Mwanza

Masista wanne wa Shirika la Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu, wamefariki dunia baada ya gari lao kugongana uso kwa uso na lori mkoani Mwanza.

Waliofariki ni pamoja na Mama Mkuu wa Shirika hilo duniani, Sista Nelina Semeoni (60), raia wa Italia.

Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa imesema ajali hiyo ilitokea Septemba 15, 2025 saa 1:50 usiku katika kijiji cha Bukumbi, Kata ya Idetemya, Wilaya ya Misungwi, barabara ya Usagara-Kigongo Feri.

Masista hao walikuwa wakielekea uwanja wa ndege wa Mwanza wakitokea Jumuiya ya Bukumbi, wilayani Misungwi.

Mbali na Sista Nelina, pia waliopoteza maisha ni msaidizi wake, Sista Lilian Kapongo (55), mkazi wa Tabora, Sista Damaris Matheka (51), Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Bukumbi na raia wa Kenya pamoja na Sista Stellamaris Muthin (48), raia wa Kenya pia na dereva wa gari walilokuwa wakisafiria, Boniphace Msonola (53).

Sista Pauline Mipata (20), Msimamizi wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Bukumbi, amenusurika kifo katika ajali hiyo na amelazwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Mwanza kwa ajili ya matibabu.

Leave a Reply