Rais Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali anayoiongoza haitakubali kupangiwa cha kufanya na mataifa ya nje, bali itaamua mambo yake kwa maslahi ya Watanzania.
Dkt Samia ameeleza hayo leo Jumanne Disemba 2,2025 wakati akihutubia Taifa katika mkutano wake na Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam jijini hapa.
Mkuu huyo wa nchi, amejenga hoja hiyo, akirejea madai ya baadhi wapinzani ambao hawakushiriki uchaguzi mkuu wakihofia kushindwa, na badala yake kutoa visingizo vinavyoungwa mkono na mataifa ya nje yanayotishia kuiwekea masharti Tanzania.
“Hawana hata aibu, nje huko wanakaa oooh… Tanzania ifanye moja, mbili, ifanye tatu, halafu ndio itakuwa hivi, ‘who are you?,” amehoji Dkt Samia huku akishangiliwa na umati wa watu waliokuwa wakimsikiliza ukumbini hapo.
“Niwaulize ndugu zangu kwao hayatokei? Tumenyanyua sauti sisi kusema ya kwao? Wanadhania bado wakoloni kwetu? kitu gani, ni fedha chache wanazotupatia? Na fedha yenyewe haipo, tunafanya biashara, wao wapate na sisi tupate, ndipo tunaposimamia,” amesema Dkt Samia.
