IMEELEZWA kuwa vigogo wajuu wa Chadema akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu na Katibu mkuu, John Mnyika wamepanga kumfukuza uanachama Lembrus Mchome, kada aliyehoji uteuzi wa viongozi wa sekretarieti na wajumbe wa kamati kuu.
Pia, vigogo hao akiwemo Godbless Lema wanadaiwa kudhamiria kumfukuza uanachama kada huyu maarufu na kumvua wadhifa wake wa uenyekiti wa wilaya ya Mwanga kwa hatua hiyo ya kuhoji uteuzi hali ambayo imezua mjadala kwenye mitandao ya kijamii na kuwagawa baadhi ya makada wa Chadema.
Ingawa bado haijajulikana rasmi ni lini lakini taratibu za kuandaa kikao cha mpango kabambe kwa ajili ya kumshughulikia Mchome zimeshakamilika, kinachosubiriwa ni wahusika kuketi kwa ajili ya ajenda moja ya kumfukuza.
Taarifa zilizopo zinaeleza kuwa endapo Mchome atafukuzwa uanachama baadhi ya makada waandamizi wakiwemo wajumbe wa baraza kuu wamesikika wakipaza sauti ya kwamba hawakubaliana na uonevu huo na kwamba watamsapoti kwa hatua atakazochukua.
“Hatutakubali kwa sababu hajafanya kosa lolote kwa hatua yake ya kuhoji. Sasa ikitokea amefukuzwa tutakuwa naye bega kwa bega hata akienda mahakamani kudai haki yake.
“Tunajua Mchome hayuko vizuri na Lema (mjumbe wa kamati kuu) pamoja na Aman Golugwa (Naibu katibu mkuu Bara) ambao walitofautiana wakiwa viongozi wa kanda ya Kaskazini. Tunajua watatumia fursa hii kumshughulikia Lembrus,” alisema mmoja wa makada.
Hivi sasa bado hakujatulia ndani ya Chadema kuna mpasuko wa viongozi na wanachama na hakuna umoja. Sasa hili la Mchome likitokea litatochochea hali kutokuwa mzuri.
Barua iliyosambaa mtandaoni jana iliyoandikwa na Mchome kwenda kwa katibu mkuu Mnyika amehoji uhalali wajumbe wa kamati kuu na sekretarieti kuthibitishwa na Baraza Kuu la Chadema lililoketi Januari 22 pasipo akidi kutimia.
Tangu kumalizika uchaguzi kumekuwa na kutunishiana misuli baina pande mbili zinazomuunga mkono Lissu na Freeman Mbowe. Kingine kinachowapa wakati mgumu Chadema ni suala la No Reforms No election ambayo miongoni mwao hawaielewi kabisa na kubaki njia panda.