You are currently viewing  EACOP, REA kunufaisha wakazi waliopitiwa na bomba la mafuta

 EACOP, REA kunufaisha wakazi waliopitiwa na bomba la mafuta

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Nishati Vijijini (REA) wamesaini randama ya kusambaza umeme katika vijiji vinavyopitiwa na mradi huo kwenye mikoa minane nchini.

Akizungumza mara baada ya kusaini makubaliano hayo jana Jumamosi jijini hapa, Mkurugenzi Mtendaji wa EACOP Tanzania, Bw. Guillaume Dulout alisema kuwa wameamua kushirikiana na REA kwa ajili ya kusaidia wananchi wanaopitiwa na bomba la mafuta, hivyo kuleta ahueni sambamba  na kulinda mazingira.

“Wananchi wa maeneo haya ni wanafamilia wa mradi huu, na sisi tumepitisha umeme kwa ajili ya kusukuma mafuta kwenye bomba letu, hivyo tumeona kwa umuhimu wao kwenye bomba letu tuwasaidie kuwapatia umeme bure,” alisema Bw. Dulout.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mradi wa Bomba la Mafuta la Afrika Mashariki (EACOP) Tanzania Bw. Guillaume Dulout (walio kaa wapili kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi. Hassan Saidy (walio kaa wapili kulia) pamoja na viongozi wa idara tofauti kutoka EACOP (waliosimama) katika hafla ya utiaji wa saini wa Mkataba wa awali (RANDAMA) unaokusudia kupeleka umeme katika vijiji vyote vilivyopitiwa na mradi huo. Waliokaa kushoto ni Zaria Nahoza Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Ndani (EACOP) na kulia ni Musa Muze Meneja wa sheria (REA)

Alisema wataanza kusambaza umeme kwa wananchi kuanzia mkoani Kagera na kuendelea mpaka mkoani Tanga kwa kuhudumia zaidi ya mitaa 17,000.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy aliipongeza EACOP kwa kuamua kuingia makubaliano ya kusambaza umeme kwa wananchi, mbali ya kunufaisha wananchi hao vilevile itasaidia utunzaji wa mazingira katika eneo zima lililopitiwa na mradi kuanzia Kagera mpaka Tanga.

“Wananchi wa maeneo haya watatumia umeme kwa ajili ya matumizi mbalimbali hususani ya kupikia, hivyo wataacha mazoea ya kutumia kuni na mkaa ambavyo vinasababisha uharibifu wa mazingira”, alisema Mhandisi Saidy.

Alisema kwamba mpango huo ni wa miaka mitano, ambapo EACOP itachangia bilioni 2.5 kwa mwaka, na REA itachangia bilioni tano kwa kila mwaka.

Naye Meneja wa Sheria wa EACOP Tanzania,  Bw. Stanley Mabiti alisema kuwa mradi huo utakuwa na tija sana kwa wananchi kwani utawainua kiuchumi kwa kuanzisha viwanda vidogo vidogo  vya uchakataji wa bidhaaa mbalimbali, hivyo kujiongezea kipato.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mradi wa Bomba la Mafuta la Afrika Mashariki (EACOP) Tanzania Bw. Guillaume Dulout (walio kaa wapili kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi. Hassan Saidy (walio kaa wapili kulia) wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi tofauti kutoka EACOP na REA (waliosimama) wakati wa hafla ya utiaji saini wa Mkataba wa awali (RANDAMA) unaokusudia kupeleka umeme katika vijiji vyote vilivyopitiwa na mradi huo.

“Mradi huu unaungana na Dira ya Taifa ya 2050 ya kuhakikisha kila mwananchi anapata nishati safi ya kupikia pamoja na shughuli zake nyingine za kimaendeleo”, alisema Bw. Mabiti.

Pamoja na hayo Bw Mabiti aliwaasa wananchi wa maeneo hayo wachangamkie fursa hiyo na fursa nyingine zote zinazotolewa katika maeneo yanayowazunguka ili kubadilisha hali za maisha yao.

“Naomba mfahamu kwamba malengo makuu ya EACOP ni kuboresha hali za kiuchumi kwa wakazi wote waliopitiwa na mradi huu kwa kutoa huduma mbalimbali za kijamii kama vile shule, maji, nishati na nyinginezo.

Wanahisa wa EACOP ni TotalEnergies yenye asilimia (62), Shirika la Maendeleo ya Petrol Tanzania (TPDC) na Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda (UNOC) yakimiliki asilimia 15 kila moja na kampuni ya mafuta ya Kichina (CNOOC) ikiwa na asilimia nane.

Bomba la EACOP, lenye urefu wa kilometa 1443, linaanzia Wilaya ya Hoima nchini Uganda na kuishia nchini Tanzania katika Mkoa wa Tanga. Bomba hilo limepita katika mikoa nane ya Tanzania bara ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga.