You are currently viewing DC Lawuo akagua miradi ya elimu Magu, atoa maagizo

DC Lawuo akagua miradi ya elimu Magu, atoa maagizo

MKUU wa Wilaya ya Magu, Jubilate Lawuo amekagua miradi ya ujenzi inayohusiana na sekta ya elimu ya msingi katika wilaya hiyo na kutoa maagizo ya kukamilisha miradi hiyo haraka.

Aidha, amekabidhi eneo lenye ukubwa wa hekari tano kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya msingi katika kijiji cha Kanyama kilichoko kata ya Bujora wilayani humo, hatua iliyopokewa kwa furaha na wananchi wa eneo hilo.

Akiwa ameongozana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya pamoja na wataalaam mbalimbali wa halmashauri, DC Lawuo leo Jumatatu amekagua maendeleo ya ujenzi wa madarasa manne na matundu 12 ya vyoo katika shule ya msingi Muungano iliyopo kata ya Kisesa.

Hata hivyo, mbali na kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa miradi hiyo ambayo imefikia hatua ya mwisho, Mkuu huyo wa wilaya amewataka wasimamizi wa miradi hiyo kuhakikisha inatekelezwa kwa ufanisi.

Aidha, akikabidhi eneo la ujenzi wa shule mpya ya msingi katika Kijiji cha Kanyama chenye wakazi zaidi ya 5000, DC Lawuo amewataka wananchi wa eneo hilo kukusanya nguvu kazi haraka kuanza ujenzi huo na serikali haitosita kuendelea pale watakapoishia kukamilisha mradi huo.

Baadhi ya wananchi wa eneo hilo akiwamo Mwenyekiti wa Kijiji cha Kanyama, Kudema Michael amemshukuru mkuu wa wilaya kwa kuhakikisha eneo hilo lenye ukubwa wa hekari tano linatengwa.

“Tulikuwa na uhitaji wa eneo hili kwa muda mrefu, tunamshukuru sana kwa hatua hii kwani itakuwa chachu kwa maendeleo ya jamii hii hasa ikizingatiwa watoto wetu wanapata changamoto mbalimbali ikiwamo kugongwa na magari wanapovuka kwenda upande wa pili kwenda shule ya msingi Kanyama,” amesema.

Katika ziara hiyo pia, Mkuu wa wilaya amekagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa na matundu sita ya vyoo katika shule ya msingi Kanyama.

Ujenzi wa miradi hiyo katika shule hiyo yenye wanafunzi 2,100, umefikia asilimia 85 huku zaidi ya Sh milioni 46 zikiwa zimetumika kati ya Sh milioni 88 zilizoletwa na Serikali kuu kupitia Mradi wa kuimarisha Ufundishaji na Ujifunzaji kwa Shule za Awali na Msingi Tanzania Bara (BOOST).

Leave a Reply