You are currently viewing Dkt. Samia atunukiwa shahada nyingine ya heshima
Rais Dkt Samia Suluhu Hassan

Dkt. Samia atunukiwa shahada nyingine ya heshima

Juhudi, maarifa na uongozi bora wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, umeendelea kumpa heshima mbele ya dunia, baada ya Chuo Kikuu cha Nasarawa nchini Nigeria kumtunuku shahada ya heshima.

Shahada hiyo ni ya saba ya heshima anatunukiwa mkuu huyo wa nchi, kwani tayari alishatunukiwa nyingine kwa nyakati tofauti katika vyuo vikuu barani Ulaya, Asia na Afrika.

Chuo Kikuu cha Nasarawa nchini Nigeria kimemtunuku Dkt Samia shahada hiyo leo, Jumamosi Aprili 11, 2026, kwa njia ya mtandao, akiwa Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma

Sababu nyingine zilizotajwa, ni uimara wa uongozi wake barani Afrika, kukuza ushirikiano wa kimataifa na kusukuma mbele maendeleo ya kiuchumi pamoja na jamii.

Akizungumza baada ya kutunukiwa shahada hiyo, Rais Dkt Samia amesema heshima aliyopewa ni ya Watanzania wote kutokana na mchango wao katika maendeleo ya Taifa na Bara la Afrika.

“Nilifurahi nilipopokea barua iliyonifahamisha kuhusu shahada hii ya heshima ambayo nimeelezwa nimeipata kutokana na mchango wangu katika maendeleo ya bara la Afrika. Naamini heshima hii si yangu peke yangu bali ni ya wananchi wote wa Tanzania, hivyo naitoa hii shahada kwa Watanzania wote,” amesema.