You are currently viewing Ufaulu sekondari Magu wazidi kupaa, walimu, wanafunzi wapongezwa

Ufaulu sekondari Magu wazidi kupaa, walimu, wanafunzi wapongezwa

Na Mwandishi Wetu, Mwanza

WALIMU na wanafunzi katika halmashauri ya wilaya ya Magu wamepongezwa kwa jitihada za kuongeza ufaulu wa mitihani kidato cha sita, nne na pili katika mwaka 2025.

Pongezi hizo zimekuja baada ya kufanikiwa kuendeleza ubora wa ufaulu kwa mitihani yote ambapo kidato cha sita umefikia asilimia 100, kidato cha nne asilimia 97.1 na kidato cha pili asilimia 91.9.

Hayo yamebainishwa leo Jumanne mjini Magu mkoani Mwanza katika hafla ya kuwapongeza walimu na wanafunzi waliochangia ubora wa ufaulu huo.

Walimu hao wamepatiwa tuzo, kombe, cheti na fedha taslimu kwa lengo la kuwapa motisha ya kuendelea kuwaanda vizuri wanafunzi kwa mitihani inayofuata.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika juzi Magu Mjini, Mkuu wa Wilaya Magu, Jubilate Lawuo amewapongeza walimu kwa kuwa taa inayoangaza vema katika sekta ya elimu wilayani humo na kuimarisha ufaulu kila mwaka.

Lawuo ambaye alikuwa ameambatana na Mkurugenzi wa Halmashauri, Mohamed Ramadhani; Mwenyekiti wa Halmashauri, Edward Kihamba amewapongeza walimu wa shule hizo kwa kuvunja mwiko wa kwamba wanafunzi wa mikoa yenye miji na majiji pekee ndio inayoweza kupata ufaulu wa juu.

Pia amewataka walimu wa shule za wilaya hiyo kumshirikisha pindi wanapokabiliana na changamoto mbalimbali ikiwamo wazazi wakaidi kuchangia chakula cha watoto wao wawapo shuleni.

Aidha, Mkurugenzi wa wilaya hiyo amepongeza kazi kubwa inayofanywa na walimu hao kwa ushirikiano na jamii hasa ikizingatiwa taaluma yao ndio msingi bora wa mtoto yeyote.

“Kufundisha wanafunzi zaidi ya 115,000 wa wilaya hii sio kazi ndogo. Wote hao wajitambue hakika ni kazi ngumu hivyo tunawapongeza sana,” amesema.

Akifafanua zaidi kuhusu ufaulu huo, Afisa Elimu Sekondari Magu, Beatrice Balige amesema ufaulu wa mtihani kitaifa  kidato cha nne ni wa kuridhisha kwani mwaka 2024 ulikuwa 97.5% na mwaka 2025 ni asilimia 97.1 huku shule 21 zikifanikiwa kufuta daraja sifuri.

“Kidato cha pili shule 48 zilifanya upimaji. Ufaulu ulikuwa asilimia 91.9.  Ufaulu umeongezeka kwa asilimia 5.2 ikilinganishwa na mwaka jana. Mwaka 2023 ilikuwa na ufaulu wa 81.89%, mwaka 2024 ufaulu ulikuwa 86.7% na mwaka 2025 asilimia 91.9,” amesema.

Kwa upande wa kidato cha sita ufaulu ni asilimia 100 huku wanafunzi waliopata daraja la kwanza mpaka la tatu pia ikiwa ni asilimia 100.

“Hapakuwa na daraja la nne wala sifuri. Shule iliyoongoza ni Magu sekondari kwa kuwa na GPA 2.4, Lugeye sekondari GPA 2.56 na Mwanza girls GPA 2.59,” amesema.

Aidha, Elias Butemi (17) ambaye ni mmoja wa wahitimu kidato cha nne katika shule ya sekondari Nyanguge, amesema siri ya ufaulu wake wa division 1.7 ni kuwasikiliza walimu na wazazi kwa umakini lakini kujisomea kwa bidii na kumuomba Mungu.

Butemi mbali na kuwashukuru walimu, wazazi na serikali kwa kuchangia mazingira bora ya elimu, ametoa wito kwa wanafunzi wa wilaya hiyo kusoma kwa bidii na kupata ufaulu mzuri.