KAMATI ya kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imeeleza kuridhishwa na utendaji kazi wa Benki ya Biashara Tanzania (TCB), huku ikiielekeza benki hiyo kuendelea kutoa gawio kwa serikali kuu ili fedha hizo zitekeleze miradi mingine ya kimkakati.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es salaam jana tarehe 16 Novemba 2024 na Mwenyekiti wa kamati hiyo Augustino Vuma wakati walipotembelea benki hiyo ili kufahamu mikakati, utendaji kazi pamoja na mwelekeo wake kwa mwaka 2025.
Amesema pamoja na mambo mengine ushirikiano wa benki hiyo na taasisi nyingine za serikali ikiwemo Shirika la Reli Tanzania -TRC, katika utoaji wa huduma imetajwa kuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi nchini.
“Ninachowasihi muendelee kuchapa kazi ili mtoe gawio kwa serikali. Kwa sababu hela mtakazozitoa zitaenda kupeleka maji, umeme na huduma nyingine mathalani katika mikoa ya Kilimanjaro au Kigoma. Kwa hiyo tunawategemea sana kama watanzania wenzetu. Tunatambua mnafanya kazi nzuri ya kuwahudumia watanzania nasi tunawasihi endeleeni hivyohivyo,” alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TCB, Adam Mihayo alisema benki hiyo itaendelea kushirikiana na serikali katika nyanja zote ikiwa ni pamoja na kijamii na kiuchumi.
“Tutaendelea kuchapa kazi kwa bidi, hivyo wafanyakazi wenzangu tusiridhike kwani matarajio ya serikali kwa taasisi hii ni kusukuma gurudumu la maendeleo ili matarajio yake yawezi kufikiwa.
“Ninachowahakikishia tutaendelea kufanya uwekezaji kwenye maeneo ya kidigitali ili kuongeza tija na kuwagusa Watanzania wengi zaidi kwa huduma rahisi na rafiki,” alisema.
Itakumbukwa kuwa Kamati hiyo imekua ikifanya ziara yake ya kutembelea taasisi mbalimbali za Serikali ili kusikiliza changamoto zao, kuona utendaji wao wa kazi na kuwasilisha ripoti kwa serikali kuu.