You are currently viewing Benki ya Dunia yaimwagia Tanzania trilioni 14 kupiga jeki elimu, kaya maskini

Benki ya Dunia yaimwagia Tanzania trilioni 14 kupiga jeki elimu, kaya maskini

Benki ya Dunia, Kupitia Bodi yake ya Wakurugenzi, imeiidhinishia Tanzania dola za Marekani milioni 550 sawa na zaidi ya shilingi trilioni 1.4 kwa ajili ya kutekeleza miradi miwili ya kimkakati katika sekta za elimu na kusaidia kaya masikini.

Uamuzi huo wa Benki umetangazwa na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Dkt. Ndiame Diop, alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, pembezoni mwa Mikutano ya Majira ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF, Makao Makuu wa Taasisi hizo Jijini Washington D.C, nchini Marekani.

Kati ya fedha hizo, dola za Marekani milioni 300 zitatumika kusaidia program ya elimu ya kuongeza ujuzi hususana kwa vijana na kiasi kingine cha dola za Marekani milioni 250 kitatumika kwa ajili ya kusaidia program ya kusaidia kaya masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF

Dkt. Diop alisema kuwa uamuzi huo unafuatia uhusiano imara uliopo kati ya Tanzania na Benki hiyo pamoja na utekelezaji mzuri wa miradi inayofadhiliwa na Benki, pamoja na usimamizi mzuri wa sera zake za uchumi na fedha.

Makamu huyo wa Rais wa Benki ya Dunia aliahidi kuwa Benki inaendelea kuchakata miradi mingine ya kimkakati iliyowasiliashwa na Tanzania kwa ajili ya kupata ufadhili wa Benki ikiwemo sekta ya nishati, kilimobiashara, miradi ya afya Zanzibar na mingine ili kuiwezesha Tanzania kufikia malengo iliyojiwekea katika kukuza uchumi na maisha ya wananchi.

Akizungumza baada ya kikao hicho, Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, aliishukuru Benki ya Dunia kwa kupitisha miradi hiyo miwili ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya nchi pamoja na majadiliamo yenye tija kwenye maeneo ya miradi muhimu ya maendeleo kwacnchi.

“Pia tumejadili kuhusu maendeleo ya ushoroba wa usafirishaji ambao ni suala muhimu pia ambapo tumeangazia namna korido ya usafirishaji ambayo nchi imewekeza kiasi kikubwa cha fedha ikiwemo reli ya SGR inavyoweza kuchochea uchumi kujumishi na endelevu” alisema Mhe. Balozi Omar.