You are currently viewing Dkt Samia: Tunafikiria kuwawezesha mitaji wafungwa wanapotoka gerezani

Dkt Samia: Tunafikiria kuwawezesha mitaji wafungwa wanapotoka gerezani

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, ametaka Serikali yake ianze kufikiria mpango wa kuanzishwa mfuko maalumu katika Jeshi la Magereza, utakaochangiwa fedha ambazo wafungwa watakaotoka gerezani na ujuzi, wapewe mitaji ya kuanzia maisha.

Dkt Samia ameyasema hayo leo, Jumamosi Mei 9, 2026 alipozungumza wakati wa hafla ya kuhitimisha mafunzo ya uongozi ngazi ya juu kozi namba 48 kwa mwaka 2025/26 katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania.

Amesema Serikali imeendekea kufanya mageuzi ya mifumo kwa kuweka kipaumbele katika urekebishaji wa tabia za wafungwa unaofungamanishwa na ujuzi na maandalizi ya mfungwa kurejea katika jamii akiwa na tabia njema na mchango kwa ustawi wa maendeleo.

Pamoja na kuwa na ujuzi, amesema changamoto inabaki wanapotoka wanakwenda kufanya nini na wanaanzaje ilihali hawana mitaji.

“Nilikuwa nanong’ona na Mkuu wa Jeshi na Waziri, kuanza sasa kufikiria sera ya kuanza kuwachangia magereza. Kuwe na mfuko maalumu kwa wale wafungwa wanaotoka na ujuzi mzuri waanze kupatiwa chochote cha kwenda kuanzia kazi,” amesema.

Ametaka magereza kufanya utafiti kuhusu sababu za wafungwa kurejea magerezani hata wanapomaliza vifungo vyao.