You are currently viewing Prof. Shemdoe: Hakuna muda wa nyongeza kwa wakandarasi

Prof. Shemdoe: Hakuna muda wa nyongeza kwa wakandarasi

Na Mwandishi Wetu, Shinyanga

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe amesema Serikali haitomuongezea muda Mkandarasi M/s China Civil Engineering Construction Corporation wa kukamilisha miradi ya ujenzi wa barabara na mitaro katika Manispaa ya Kahama.

Ujenzi huo unatekelezwa kupitia Mradi wa Uendelezaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) kutokana na ubovu wa miundombinu ya barabara kuwa kero ya muda mrefu kwa wananchi wa manispaa hiyo.

Prof. Shemdoe amesema hayo jana Mei 27, 2026 katika Manispaa ya Kahama wakati wa hafla ya Utiaji Saini wa Mkataba wa Umaliziaji wa Ujenzi wa Barabara na Mitaro kupitia Mradi wa TACTIC iliyofanyika katika eneo la Phantom kwenye manispaa hiyo.

Sanjari na hilo, Prof. Shemdoe amemtaka Mtaalamu Mshauri kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama pamoja na TARURA katika kuhakikisha mikataba iliyosainiwa inatekelezwa kikamilifu na inakamilika ndani ya muda uliopangwa na kwa ubora uliokubalika ili thamani ya fedha ionekane.

Prof. Shemdoe amesema imekuwa ni siku yenye furaha kwani kitendo cha kusainiwa kwa mikataba hiyo kinasadifu nia ya dhati ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwaboreshea miundombinu ya barabara wananchi wa Kahama na kuongeza kuwa kama lilivyo jina lake amekuwa ni suluhu ya changamoto iliyokuwa ikiwakabili wananchi wa manispaa ya Kahama.

Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita amesema Manispaa ya Kahama inatekeleza mradi wa TACTIC kwa awamu mbili, awamu ya kwanza inahusisha ujenzi wa barabara za katikati ya mji (Central Business District (CBD) zenye urefu wa Kilomita 12.3 na barabara ya eneo la Zongomela kilomita tatu (3) pamoja na ujenzi wa mfereji wa maji ya mvua wa Chelsea–Lyazungu, Shunu–Magobeko (Standalone Storm Water Drain).

Naye, Mratibu wa Miradi ya Ushirikiano na Benki ya Dunia, Mhandisi Humprey Kanyenye wa TARURA amesema kuwa, mkandarasi huyo anakwenda kutekeleza mradi huo katika Manispaa ya Kahama kwa gharama ya Shilingi Bilioni 25.5 na utatekelezwa kwa muda wa miezi nane (8) kuanzia Juni 01, 2026 hadi Januari 31, 2027.