Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, amesema Jeshi la Polisi linapaswa kuonekana likifuata miiko na kuepuka mambo yanayokatazwa wakati wa utekelezaji wa kazi zake ili kuwa na ufanisi, kukuza tija na kufikia malengo yanayokusudiwa.
Amesema ni vyema wananchi washirikishwe kwenye polisi jamii ili wasimamie wenyewe usalama wao na kuamini Jeshi la Polisi ni kimbio la shida zao.
Rais Dkt Samia ameeleza hayo, leo Mei 28, 2026 wakati akihitimisha Mafunzo ya Maofisa na Wakaguzi Wasaidizi wa Polisi, Kurasini, Dar es Salaam leo Mei 28, 2026.
Amesema anapeda kuona matokeo, ni uwezo wa Jeshi la Polisi kutambua viasharia vya hatari vya usalama kwa nchi mapema iwezekanavyo.
“Mfano tulikuwa tunapokea Ripoti ya Matukio ya Oktoba 29, 2025, walisema labda uzoefu mila na desturi zetu kwamba Tanzania ni nchi ya amani, nchi ya usalama na kwamba vikitokea vitisho hatuvipi uzito wake, tunasema aah watatukuta asubuhi tunapiga mswaki, kwahiyo wakija sisi tupo bwana,”amesema na kuongeza.
“Yaliyotokea yametupa funzo, tulijaribiwa na kwa dhati nishukuru vyombo vya ulinzi na usalama, majaribio yale waliweza kuyaondoa ndani ya muda mfupi sana,” amesema.
