You are currently viewing EACOP, TotalEnergies wawajengea uwezo wanafunzi 200 kutambua fursa sekta ya nishati
Screenshot

EACOP, TotalEnergies wawajengea uwezo wanafunzi 200 kutambua fursa sekta ya nishati

Na Mwandishi Wetu, Arusha

Katika juhudi za kuhakikisha sekta ya nishati inachangia kikamilifu ukuaji wa uchumi wa taifa, Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kwa kushirikiana na wanahisa wakuu wa mradi huo, TotalEnergies umeendelea kuwawezesha vijana kupitia makongamano, semina na mafunzo mbalimbali yanayowawezesha kutambua na kunufaika na fursa zilizopo katika sekta hiyo hapa nchini.

Screenshot

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Nne la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu mkoani Arusha, Mkurugenzi wa Shughuli za Uendeshaji wa EACOP, Bw. Paul Hiegel, alisema lengo la kongamano hilo ni kujadili nafasi ya vijana katika maendeleo ya sekta ya nishati pamoja na kuwapatia maarifa kuhusu fursa zinazotokana na uwekezaji mkubwa unaoendelea nchini katika sekta ya mafuta na gesi.

“Tunatambua kuwa vijana ndiyo nguvu kazi ya sasa na ya baadaye. Kupitia kongamano hili tunalenga kuwahamasisha kutumia fursa zilizopo katika sekta ya nishati na kujitayarisha kuwa sehemu ya maendeleo makubwa yanayoendelea nchini,” alisema Bw. Hiegel.

Alisema mradi wa EACOP umefikia hatua muhimu ya maendeleo kwa kuanza kuhama kutoka awamu ya ujenzi kuelekea awamu ya uendeshaji, hatua inayotarajiwa kuanza katika siku zijazo.

“Mradi umefanikiwa kuwashirikisha Watanzania wengi katika nafasi mbalimbali za ajira na uongozi, jambo linaloonesha dhamira ya kuwawezesha wananchi kunufaika moja kwa moja na uwekezaji huu,” aliongeza.

Bw. Hiegel alisisitiza kuwa mafanikio ya mradi hayapaswi kupimwa kwa miundombinu inayojengwa pekee, bali pia kwa urithi wa maarifa, ujuzi na fursa utakaoachwa kwa jamii na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Ushirikishwaji wa Wadau na Utetezi kutoka TotalEnergies, Bi. Marieme-Sav Sow, alisema kongamano hilo limewapa wanafunzi fursa ya kipekee ya kujifunza moja kwa moja kutoka kwa wataalamu na viongozi waandamizi wanaosimamia miradi mikubwa ya kimkakati.

“Mbali na kupata maarifa, wanafunzi wameweza kujenga mitandao ya kitaaluma kwa kukutana na viongozi waandamizi wanaohusika katika utekelezaji wa miradi mikubwa, jambo ambalo mara nyingi halipatikani kwa urahisi kwa vijana wengi,” alisema Bi. Sow.

Aliongeza kuwa vijana wana nafasi kubwa ya kuwa wataalamu, wabunifu na wajasiriamali katika sekta ya nishati, hivyo ni muhimu kuendelea kuwapa elimu na taarifa sahihi zitakazowawezesha kufanya maamuzi yenye manufaa kwa maisha yao na maendeleo ya taifa.

Bi. Sow alisema kongamano hilo limewakutanisha wanafunzi zaidi ya 200 kutoka vyuo mbalimbali, ikiwemo Chuo cha Ufundi Arusha  (ATC), Chuo cha Nelson Mandela cha Sayansi na Teknolojia (NM-AIST) na Chuo Cha Uhasibu Arusha (IAA).

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Mipango na Uwekezaji kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli  nchini (TPDC), Bw. Derick Moshi, alisema kongamano hilo limewapa wanafunzi uelewa mpana kuhusu matarajio ya sekta na mahitaji ya miradi ya mafuta na gesi kuanzia hatua ya ujenzi hadi uendeshaji.

“Matukio ya aina hii yana mchango mkubwa katika kuwaandaa wanafunzi kwa maisha ya kazi baada ya kuhitimu masomo yao. Yanawapa fursa ya kujifunza kuhusu sekta ya mafuta na gesi na namna wanavyoweza kushiriki katika mnyororo mzima wa thamani wa sekta hiyo,” alisema Bw. Moshi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Masomo wa Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), Dkt. Nicodemus Mbwambo, alisema kongamano hilo limeendelea kuwa jukwaa muhimu linalowaunganisha wadau wa sekta ya nishati, taasisi za elimu ya juu na wanafunzi kwa lengo la kujadili fursa na maendeleo yanayoendelea katika sekta hiyo.

“Tunathamini ushirikiano huu unaowawezesha wanafunzi kupata maarifa, ujuzi na uzoefu unaohitajika katika soko la ajira. Lengo letu ni kuona vijana wetu wanahitimu wakiwa tayari kushiriki katika fursa mbalimbali zinazotokana na miradi mikubwa ya kimkakati kama EACOP na sekta nzima ya nishati,” alisema Dkt. Mbwambo.

Baadhi ya wanafunzi walioshiriki kongamano hilo walieleza kuwa limewapa mwanga mpya kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya nishati, wakisema elimu waliyoipata itawasaidia kupanga kwa ufanisi mustakabali wao wa kitaaluma na kiuchumi.

Kongamano hilo ni sehemu ya jitihada za EACOP na TotalEnergies, kwa kushirikiana na Ubuntu Impact Limited  za kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya rasilimali watu kwa kuwajengea vijana maarifa na ujuzi unaohitajika ili kunufaika na fursa zinazotokana na ukuaji wa sekta ya nishati nchini.

Mradi wa EACOP unamilikiwa na TotalEnergies yenye asilimia 62 ya hisa, huku Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Shirika la Mafuta la Taifa la Uganda (UNOC) vikimiliki asilimia 15 kila kimoja, na Kampuni ya Mafuta ya Taifa ya China (CNOOC) ikimiliki asilimia 8 ya hisa za mradi huo.