Imekuwa kama mtoko wa sikukuu kwa familia mbalimbali jijini Dar es Salaam, baada ya Serikali kuandaa maeneo maalumu kwa wananchi kuangalia mechi ya fainali ya mataifa bingwa Afrika kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 17.
Katika maeneo mbalimbali ya Jiji hilo, Televisheni kubwa zimefungwa mitaani kutoa nafasi kwa wananchi kuangalia mechi hiyo ya fainali inayoihusisha timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17 ya Tanzania ‘Serengeti Boys’ dhidi ya Senegal.
Mbali na wananchi katika maeneo hayo, viongozi mbalimbali wa Serikali ngazi za Mikoa na Wilaya, wameshuhudiwa wakikusanyika sambamba na wananchi kufuatilia mechi hiyo, inayoiweka Tanzania katika ramani ya soka duniani.
Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, alitoa ndege maalumu kuwabeba wachezaji na mashabiki kwa ajili ya kwenda kuishabikia timu hiyo ya vijana.
Hata hivyo, Dkt Samia pia alitoa Sh500 milioni kama motisha kwa vijana hao, baada ya kufanikiwa kuingia hatua ya fainali ya michuano hiyo
Amani na utulivu umetawaka katika maeneo hayo, wananchi wakifuatilia mechi hiyo.
