You are currently viewing DED Magu asisitiza kuwekeza nguvu kwenye michezo

DED Magu asisitiza kuwekeza nguvu kwenye michezo

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Mohamed Ramadhani ameiagiza idara ya elimu sekondari na msingi kuendelea kushirikiana kuibua vipaji vya wanafunzi na kuvilea ili waweze kufanya vizuri katika sekta mbalimbali za michezo na kitaaluma.

DED Ramadhani ametoa wito huo leo Ijumaa wakati akipokea makombe ya ushindi wa jumla katika Mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Sekondari Tanzania (UMISETA) 2026 ngazi ya wilaya yaliyofanyika mwezi uliopita jijini Mwanza.

Katika mashindano hayo, halmashauri ya wilaya ya Magu, ilishika nafasi ya tatu na kubeba makombe 10 ikilinganishwa na mwaka jana ambapo ilishika nafasi ya tano na makombe saba.

Akizungumza na walimu, makocha, waratibu na viongozi wa idara hiyo ya elimu sekondari, Mkurugenzi huyo amesisitiza kuwa michezo sasa ni ajira hivyo walimu wawapokee watoto na kuwalea vizuri ili waoneshe vipaji vyao.

“Watoto tuliowaandaa shule ya msingi, wanapofika sekondari tunapaswa kuwapokea na kuendeleza vipaji vyao. Niwaombe walimu tuwapokee watoto wanaotoka msingi na kuwaendeleza. Kwa sababu akifanya vizuri kwenye michezo hata kiakili atafanya vizuri.

“Michezo inakuja juu, najaribu kuangalia matajiri duniani… hakuna tajiri mtumishi wa umma, lakini matajiri wanamichezo wapo tena wa kutosha. Michezo ni sekta ya nne inayota matajiri duniani. Pamoja na kwamba wanatokeza mmoja mmoja sana lakini bado fursa zake ni kubwa,” amesema.

Aidha, amewapongeza kwa kupiga hatua katika sekta hiyo ya michezo. “Miaka zaidi ya miwili tumekuwa watano, nawashukuru kwa mapambano yenu na namna mlivyoshirikiana kupiga hatua na kuwa watatu lakini sasa kuna vitu mnatakiwa kuviboresha,” amesema DED Ramadhani.

Awali akitoa taarifa kwa mkurugenzi, Afisa Elimu Sekondari wilaya ya Magu, Beatrice Balige amesema mbali na kupata makombe hayo 10, pia walimu wamepata uzoefu kwa sababu walikaa kwenye kambi siku 10.

“Pia tulienda kambi ya mkoa na kukaa siku tano. Tuliwapeleka pia kwenye kambi ya Taifa na mafanikio yanaonekana kwa sababu mwaka jana tulimpekeka Magdalena nchini Marekani baada ya kupata ufadhili wa kuendeleza vipaji vyake alivyovionesha kutoka shule ya Joseph&Marry,” amesema.