Na Mwandishi Wetu, Morogoro
Jumla ya vijana 588 wanaonufaika na mpango wa ufadhili wa mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana wa ‘NBC Wajibika Scholarship’ wameanza rasmi mafunzo yao katika vyuo vya VETA Kihonda mkoani Morogoro na VETA Mwanza, huku Benki ya NBC ikisisitiza dhamira yake ya kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya rasilimali watu kama njia ya kuchochea ukuaji wa uchumi jumuishi nchini.
Mpango huo unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Benki ya NBC na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), ukiwa na lengo la kuwawezesha vijana kupata ujuzi unaowawezesha kujiajiri, kuajiriwa na hata kuwa waajiri, sambamba na kuunga mkono jitihada za Serikali za kujenga uchumi shindani unaotegemea nguvu kazi yenye ujuzi, ubunifu na tija.

Hafla ya uzinduzi wa utekelezaji wa mpango huo ilifanyika jana katika Chuo cha VETA Kihonda, ambapo wanafunzi 294 wanapatiwa mafunzo, huku idadi kama hiyo ikinufaika katika Chuo cha VETA Mwanza. Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa VETA wakiongozwa na Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Mashariki, Bw. John Mwanja, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Mkuu wa Chuo cha VETA Kihonda, Dkt. Ulimwengu Salumu, walimu, wanafunzi wanufaika pamoja na maofisa wa NBC wakiongozwa na Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Mahusiano kwa Umma, Bw. Godwin Semunyu.
Kupitia mpango huo, NBC imetoa ufadhili wa zaidi ya shilingi milioni 150 kwa ajili ya kugharamia mafunzo ya muda mfupi kwa vijana hao katika fani za Ufundi Umeme, Ufundi Bomba pamoja na Ubunifu, Ushonaji na Teknolojia ya Nguo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Bw. Semunyu alisema kuwa uwekezaji wa NBC katika elimu ya ufundi stadi unalenga kuwawezesha vijana kujenga mustakabali wao wa kiuchumi na wakati huo huo kuchangia maendeleo ya taifa.
“Mbali na uwekezaji wetu katika sekta za afya, elimu na michezo, suala la ajira kwa vijana ni eneo muhimu tunalolipa kipaumbele. Takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wana umri wa chini ya miaka 35. Hii ni rasilimali kubwa inayohitaji kupewa maarifa na ujuzi ili iweze kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya uchumi wa nchi,” alisema.
Aliongeza kuwa ongezeko la wahitimu wanaoingia katika soko la ajira kila mwaka linaifanya elimu ya ufundi stadi kuwa mojawapo ya suluhisho muhimu katika kukuza ajira, ubunifu na kujitegemea kiuchumi.
“Tunaamini kuwa elimu ya ufundi stadi ni daraja muhimu la kuwawezesha vijana kujenga maisha yao kupitia ujuzi unaotambulika na unaohitajika katika soko la ajira la sasa. Ndiyo maana tunaendelea kuwekeza katika mipango yenye matokeo ya moja kwa moja kwa jamii,” aliongeza.
Aidha, aliwataka wanafunzi wanaonufaika na ufadhili huo kutumia kikamilifu fursa waliyoipata kwa kujifunza kwa bidii ili waweze kuhitimu wakiwa na maarifa, ujuzi na umahiri unaohitajika katika mazingira ya kisasa ya kazi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Mashariki, Bw. John Mwanja, aliipongeza NBC kwa mchango wake katika kuendeleza elimu ya ufundi stadi nchini, akisisitiza kuwa ushiriki wa sekta binafsi ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha mafunzo yanayoandaliwa yanaendana na mahitaji halisi ya soko la ajira.
“Ushirikiano kati ya sekta binafsi na taasisi za mafunzo ni nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa. Kupitia ushirikiano huo tunaweza kubaini mahitaji ya soko la ajira, kuboresha mazingira ya kujifunzia, kuongeza fursa za mafunzo kwa vitendo na kuimarisha uwezekano wa wahitimu kupata ajira au kujiajiri,” alisema.
Naye Mkuu wa Chuo cha VETA Kihonda, Dkt. Ulimwengu Salumu, alisema kuwa mafunzo hayo ya miezi mitano yalianza rasmi Mei 25 mwaka huu na yanajumuisha masomo ya nadharia pamoja na mafunzo kwa vitendo ili kuwajengea wanafunzi uwezo wa kufanya kazi katika mazingira halisi ya uzalishaji.
Alisema mbali na stadi za kitaaluma, wanafunzi hao pia wanapatiwa mafunzo ya ujasiriamali na stadi za maisha ili kuwawezesha kuanzisha na kusimamia biashara zao pamoja na kujenga mahusiano bora katika jamii.
“Tuna matarajio makubwa kuwa wahitimu wa programu hii watakuwa na uwezo wa kushindana katika soko la ajira, kujiajiri na kuchangia kikamilifu maendeleo ya uchumi wa taifa,” alisema Dkt. Ulimwengu.
Baadhi ya wanafunzi wanaonufaika na mpango huo walieleza shukrani zao kwa NBC, VETA na Serikali kwa kuwapatia fursa hiyo, wakisema mafunzo hayo yanakwenda kuwafungulia njia mpya za kutimiza ndoto zao za kujitegemea kiuchumi kupitia ujuzi wa ufundi stadi.
“Tunawasjukuru sana NBC kwa kubuni na kuona umuhimu wa program hii. Matarajio yetu baada ya kuhitimu ni kuanzisha shughuli zetu binafsi za uzalishaji mali, kujiajiri na hatimaye kuwaajiri vijana wengine katika jamii,” alisema mmoja wa wanufaika, Peter Lwana, kauli iliyoungwa mkono na wenzake Penina Nilanga, Fauzia Kassim na William Amon.
