Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis amelazwa hospitali kwa siku ya nne mfululizo katika kile viongozi mjini Vatican wamesema anapatiwa matibabu ya maambukizi kwenye njia ya hewa lakini anaendelea vizuri.
Papa Francis ambaye amekuwa akisumbuliwa na maradhi hayo kwa karibu wiki nzima amelazwa kwenye hospitali ya Gemelli mjini Roma tangu Ijumaa iliyopita.
Taarifa ya ofisi yake imesema madaktari walimshauri kupumzika na jana Jumapili hakuweza kuongoza misa ya kila wiki kwenye kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.
Baba Mtakatifu alifanyiwa upasuaji wa kuondoa moja ya mapafu yake alipokuwa kijana na tangu wakati huo yumo kwenye hatari ya kupata maambukizi ya mara kwa mara ya njia ya hewa.
Hata hivyo hali ya afya yake imekuwa ikifuatiliwa kwa karibu miaka ya hivi karibuni kutokana na taarifa za kuugua karibu kila wakati.