MOSCOW, URUSI
RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema dunia inapita katika kipindi cha mabadiliko makubwa kwenye sekta ya elimu ambayo yameibua fursa kwa vijana walio tayari kujifunza.
Akizungumza mara baada ya kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Uzamivu na Chuo Kikuu cha Urafiki cha Watu wa Urusi (RUDN) jijini Moscow leo, Samia alisema suala si kuamua au kuacha kujitosa katika dunia hii mpya lakini ni kwa jinsi vipaji vinaweza kuunganishwa ili kufaidika na fursa zilizopo.
“Tunapita katika dunia yenye mambo ya akili mnemba (AI), sayansi za mashine na maroboti na mabadiliko. Hakuna taifa linataka kuachwa nyuma katika hili lakini kikubwa ni kuwa tayari kujifunza na kutumia vizuri fursa zilizopo,” alisema.
Katika hotuba yake iliyokuwa ikikatizwa kwa makofi mara kwa mara, Rais Samia alisema umuhimu wa elimu umekuwa wa kudumu duniani kote, akisema umekuwa chanzo cha mabadiliko kuanzia ngazi za familia hadi taifa.
Tukio hilo lilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Sayansi na Elimu ya Juu wa Urusi, Konstantin Mogilevsky, ambaye katika hotuba yake alisema Rais Samia ametoa mchango mkubwa katika ukuzaji wa elimu nchini kwake katika kipindi cha miaka yake sita madarakani.
RUDN imekuwa na mahusiano ya muda mrefu na Tanzania, kikiwa kimesomesha zaidi ya Watanzania 1,100 tangu kianzishwe mwaka 1960 iliyopita na sasa wanafunzi wa Kitanzania 72 wanapata mafunzo katika ngazi mbalimbali chuoni hapo.
Rais Samia anakuwa Rais wa karibuni zaidi kupewa heshima hiyo na chuo hicho, huku marais wengine sita wakiwa wamewahi kupewa tuzo hiyo. Baadhi ya marais hao ni Sam Nujoma wa Namibia, Thabo Mbeki wa Afrika Kusini na Olesegun Obasanjo wa Nigeria.
Vyuo vikuu vingine saba ambavyo vimewahi kumtunukia Rais Samia shahada za namna hiyo ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Jawahral Nehru nchini India, Chuo Kikuu cha Ankara nchini Uturuki, Nasarawa nchini Nigeria, Chuo Kikuu cha Anga cha Korea Kusini, Chuo Kikuu cha Mzumbe na Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA).
