Rais Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali itaendelea kutekeleza mageuzi yanayolenga kuhakikisha kunakuwepo utulivu na uhakika utakaovutia uwekezaji nchini.
Kwa mujibu wa Dkt Samia, kupitia Mamalaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (Tiseza), Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya uratibu wa pamoja ambayo kwa sasa kusajili kampuni ni ndani ya saa 24 tofauti na hapo awali.
Dkt Samia ameyasema hayo leo, Jumanne Juni 9, 2026 alipozungumza katika Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Singapore lililofanyika jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa nchi, amesema mafanikio ya kongamano hilo hayatapimwa kwa hotuba zitakazotolewa, bali kwa ushirikiano, uwekezaji na miradi itakayozaliwa kutokana na majadiliano.
“Mafanikio ya kongamano hili la biashara hayatapimwa kwa hotuba tunazotoa leo, bali kwa ushirikiano, uwekezaji na miradi itakayoibuka kutokana na mkutano huu,” amesema.
Rais Samia amewahimiza washiriki kutoka serikalini na sekta binafsi kutumia fursa hiyo kujadiliana kwa kina na kukubaliana hatua za vitendo zitakazoimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Singapore.
“Kwa hiyo, ninawahimiza washiriki wote kutoka serikalini na sekta binafsi kutumia vyema fursa hii ya kujadiliana na kwa pamoja kukubaliana hatua zinazofuata katika kuimarisha ushirikiano wetu,” amesema.
Amesisitiza kuwa Serikali yake itaendelea kudumisha mazingira yenye utulivu, yanayotabirika, yenye faida kwa wawekezaji na yanayohamasisha uwekezaji wenye tija na ushirikiano wa muda mrefu.
“Serikali yangu imejidhatiti kuendelea kudumisha mazingira thabiti, yenye faida, yanayotabirika na rafiki kwa wawekezaji, yanayothamini ushirikiano wa muda mrefu na uwekezaji wenye uwajibikaji,” amesema.
