You are currently viewing Watumishi MAGU DC wapatiwa mafunzo kuongeza utayari  kukabiliana na magonjwa ya mlipuko

Watumishi MAGU DC wapatiwa mafunzo kuongeza utayari  kukabiliana na magonjwa ya mlipuko

Na Mwandishi Wetu

Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu wamepewa mafunzo maalum ya utayari wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo ugonjwa wa Ebola kufuatia kuwepo kwa milipuko ya ugonjwa huo katika nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Uganda.

Mafunzo hayo yalilenga kuongeza uelewa kwa watumishi namna ya kutambua dalili za Ebola, jinsi ugonjwa huo unavyoenea pamoja na mbinu sahihi za kujikinga ili kuzuia maambukizi katika jamii.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mratibu Kinga na Magonjwa ya Mlipuko wilaya ya Magu, Elywitness Rwoto amesema kuwa Ebola ni miongoni mwa magonjwa hatari ya mlipuko yenye kiwango kikubwa cha vifo endapo hatua za haraka hazitachukuliwa.

Ameeleza kuwa hadi sasa ugonjwa huo bado hauna tiba maalum inayoua virusi moja kwa moja, hivyo kinga na tahadhari ndiyo silaha kuu ya kuuzuia.

Katika mafunzo hayo, washiriki walifundishwa kuwa Ebola huenea kupitia kugusana na majimaji ya mwili wa mtu aliyeambukizwa kama damu, jasho, mate, matapishi au mkojo.

Pia walikumbushwa umuhimu wa kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni, kutumia vifaa vya kujikinga wanapohudumia wagonjwa na kutoa taarifa mapema kwa mamlaka za afya pindi wanapobaini mtu mwenye dalili zinazofanana na Ebola.

Dalili kuu za ugonjwa huo ni pamoja na homa kali ya ghafla, maumivu ya kichwa, uchovu mkubwa wa mwili, kutapika, kuharisha, maumivu ya misuli na wakati mwingine kutokwa damu sehemu mbalimbali za mwili.

Aidha, Mganga Mkuu wa wilaya ya Magu, Dk. Raphael Mhana aliwataka wananchi kuepuka kugusa mizoga ya wanyama na miili ya watu waliofariki kwa ugonjwa usiojulikana bila kutumia vifaa vya kinga, pamoja na kuepuka safari zisizo za lazima katika maeneo yenye milipuko mikubwa ya ugonjwa huo.

Mafunzo hayo yanaelezwa kuwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuendelea kuimarisha mifumo ya tahadhari na ufuatiliaji wa magonjwa ya mlipuko ili kuhakikisha wananchi wanabaki salama dhidi ya tishio la Ebola.