You are currently viewing Dkt Samia: Tunashirikiana na Urusi kujenga ujuzi wa sayansi, teknolojia nchini

Dkt Samia: Tunashirikiana na Urusi kujenga ujuzi wa sayansi, teknolojia nchini

Rais wa Samia Suluhu Hassan, ameeleza kuwa ushirikiano wa kimkakati kati ya Tanzania na Urusi unaelekezwa katika vipaumbele muhimu vya maendeleo ya Taifa vinavyoendana na Dira ya muda mrefu ya maendeleo ya nchi.

Ameeleza hayo katika mahojiano wakati wa ziara yake jijini Moscow,  Rais Samia amesema Tanzania na Urusi, zimefanikiwa kubaini kati ya sekta sita hadi tisa za kipaumbele  zinazoakisi ajenda ya maendeleo ya muda mrefu ya Tanzania pamoja na mfumo wa ushirikiano wa Urusi.

Kwa mujibu wa Dkt Samia, maeneo hayo yanajumuisha kilimo, madini, nishati, afya, elimu na mageuzi ya kidijitali, akibainisha kuwa sekta hizo ni nguzo muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya miaka 25 kuanzia mwaka 2025 hadi 2050.

Rais Samia alisema miongoni mwa maeneo yanayopewa kipaumbele katika ushirikiano huo ni pamoja na mifumo ya serikali mtandao (e-Government) kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma za umma.

Amefafafanua kuwa serikali inalenga kutumia teknolojia ya kidijitali katika shughuli zake ili kuhakikisha huduma zinawafikia Watanzania kwa urahisi zaidi bila kujali walipo.

“Tunazingatia maendeleo ya Serikali mtandao kwa ajili ya kufanya shughuli za serikali kwa mfumo wa kidijitali ili tuweze kumhudumia kila Mtanzania popote alipo,” amesema.

Mbali na hilo, Dkt Samia amesema  ushirikiano huo pia unalenga kuimarisha ujenzi wa uwezo wa rasilimali watu katika nyanja za sayansi na teknolojia.

Katika mahojiano hayo, Dkt Samia ameyataja maalumu kama sayansi ya nyuklia, ambayo yana umuhimu mkubwa kutokana na uwepo wa rasilimali za urani nchini na matarajio ya Tanzania katika maendeleo ya sekta ya nishati siku zijazo.

Aidha, amesema ushirikiano huo unaigusa sekta ya afya kwa kuzingatia mafunzo ya wataalamu wa sayansi za afya, uimarishaji wa utaalamu wa kitabibu na kuongeza uwezo wa nchi katika kutoa huduma bora za afya kwa wananchi.

Kimsingi, ushirikiano kati ya Tanzania na Urusi unatarajiwa kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kupitia uwekezaji, uhamishaji wa teknolojia, pamoja na ukuzaji wa ujuzi na utaalamu katika sekta mbalimbali za kimkakati.