You are currently viewing Rais Samia: Tutatumia sekta ya kilimo kama msingi wa kukuza biashara

Rais Samia: Tutatumia sekta ya kilimo kama msingi wa kukuza biashara

Rais wa Samia Suluhu Hassan amesema sekta ya kilimo inatarajiwa kuwa nguzo muhimu katika kukuza biashara na ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Urusi kwa miaka ijayo.

Akizungumza katika mahojiano wakati wa ziara yake jijini Moscow, Rais Samia alisema ushirikiano uliopo  kati ya kampuni za Tanzania na Urusi kwenye sekta ya kilimo umeweka msingi imara wa kuongeza wigo wa biashara kati ya nchi hizo mbili.

Amesema baadhi ya kampuni za Urusi tayari zinashiriki katika shughuli za uzalishaji wa mazao ya kilimo nchini ikiwemo kilimo cha ndizi, hatua inayoongeza mauzo ya zao hilo katika soko la nchi yao.

“Tunatarajiwa kuwa na ongezeko kubwa la mauzo ya ndizi kutoka Tanzania kwenda Urusi,” amesema Dkt Samia.

Mbali na hilo, Dkt Samia ameutaja uzalishaji wa mafuta ya kupikia kuwa moja ya maeneo yenye fursa kubwa za ushirikiano kati ya Tanzania na Urusi.

Ameeleza kuwa juhudi hizo zinaendelea kuimarisha minyororo ya thamani katika sekta ya kilimo na biashara ya mazao ya kilimo ili kuongeza tija na mapato kwa pande zote mbili.

Dkt Samia amesema ushirikiano huo utajumuisha programu za kuimarisha usalama wa chakula kupitia uzalishaji wa mazao mbalimbali pamoja na maendeleo ya sekta ya mifugo.

Kwa mujibu wa Rais Samia, Tanzania ina maeneo makubwa ya ranchi na malisho yanayoweza kuvutia uwekezaji kutoka Urusi katika sekta ya mifugo, jambo litakalosaidia kuongeza uzalishaji, kuimarisha biashara na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Sekta ya kilimo inaonekana kuwa moja ya maeneo muhimu yatakayochochea ongezeko la biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Urusi katika kipindi kijacho.