Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Rais Dkt Samia Suluhu Hassan Jumamosi amepokea Rais wa Namibia, Dkt Netumbo Nandi-Ndaitwah, katika Ikulu ya Dar es Salaam, ikiwa ni mwanzo wa ziara ya kitaifa ya siku tatu inayolenga kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Namibia.
Rais amepolelewa leo Juni 20,2026 kwa heshima zote za kitaifa, ikiwemo gwaride la heshima na mizinga 21, katika hafla iliyoonesha uhusiano wa karibu na wa kihistoria uliopo kati ya nchi hizo mbili.
Dkt Samia na Rais Nandi-Ndaitwah wanatarajiwa kufanya mazungumzo yatakayolenga kuimarisha ushirikiano katika maeneo mbalimbali yenye manufaa kwa pande zote.
Pia, wanatarajiwa kushuhudia utiaji saini wa mikataba kadhaa ya makubaliano (MoU), kisha kufanya mkutano na waandishi wa habari kwa pamoja.
Mbali na shughuli rasmi za kiserikali, ziara hiyo ina pia mwelekeo wa kihistoria na binafsi, ambapo Rais Nandi-Ndaitwah, aliyewahi kuishi na kufanya kazi Tanzania wakati wa harakati za ukombozi, anatarajiwa kutembelea maeneo yenye umuhimu wa kihistoria, ikiwemo Magomeni jijini Dar es Salaam na makaburi ya Wapigania Uhuru wa Namibia yaliyopo Kongwa, Dodoma.
Pia, atatembelea Kambi ya Wapigania Uhuru wa Harakati za Ukombozi wa Afrika iliyopo wilayani Kongwa kabla ya kumaliza ziara yake ya kitaifa Jumatatu, huku nchi hizo mbili zikiendelea kuimarisha urafiki na ushirikiano wa muda mrefu uliowahi kuzikutanisha katika historia ya mapambano ya ukombozi barani Afrika.
