Na Mwandishi Wetu, Moshi
Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inasogeza karibu huduma zote za afya ikiwemo ya saratani ili kurahisisha matibabu bingwa kwa Watanzania.
Dkt Samia ameeleza hayo Juni 24,2026 wakati akizindua jengo la tiba ya mionzi kwa wagonjwa wa saratani katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro.

Amesema uwepo wa tiba hiyo mkoani humo utawapunguzia gharama wananchi na kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo katika mikoa ya Dar es Salaam (Ocean Road) na (Bugando)Mwanza.
“Huu ndio mwelekeo wa Serikali wa kupunguza umbali kati ya wananchi na huduma za kibingwa wanazostahiki kuzipata. Huduma hizi kubwa kansa na upasuaji wa moyo nayo tumeanza kusogeza kwa wananchi,” amesema Rais Samia na kuongeza kuwa;
“Tulikuwa na kituo kimoja pale Ocean Road, tukapeleka Bugando na sasa kipo Kanda ya Kaskazini, tumemaliza kazi inaendelea.Tunajipanga kusogea kwenye kanda nyingine za Tanzania, lengo ni kusogeza huduma hizi karibu na wananchi,” amesema.
