You are currently viewing Samia: Tanzania ni kituo cha biashara na lango la masoko ya Afrika

Samia: Tanzania ni kituo cha biashara na lango la masoko ya Afrika

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) yameendelea kuiimarisha Tanzania kama kituo cha biashara na uwekezaji barani Afrika na duniani.

Rais Samia amesema hayo leo, Julai 3, 2026, wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam, uliofanyika jijini Dar es Salaam, ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Msumbiji, Daniel Chapo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi zawadi mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Mheshimiwa Daniel Francisco Chapo katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam, tarehe 03 Julai, 2026.

“Tunapoadhimisha miaka 50 ya maonesho haya, hatusherehekei tu maonesho yenyewe, bali pia juhudi za wafanyabiashara na wajasiriamali wetu, ubunifu wa sekta binafsi, mchango wa viwanda vyetu na nafasi ya Tanzania katika biashara ya kikanda na kimataifa inayochochea ukuaji wa uchumi wa taifa letu,” amesema Rais Samia.

Amesema ameridhishwa na mwitikio mkubwa wa washiriki wa maonesho ya mwaka huu, waliotoka ndani na nje ya nchi, zikiwemo China, Oman na Indonesia.

“Maonesho haya ni jukwaa muhimu la biashara na pia ni ishara kuwa Tanzania inaendelea kuamini kama kituo kikuu cha uwekezaji na biashara na lango la kufikia masoko katika ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Bara la Afrika na duniani kote,” amesema.