Uongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), umeanza kuvurugana, baada ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho bara, John Heche, kutafuna mamilioni ya michango wanayokusanya kutoka kwa wadau.
Chama hicho, kimekuwa kikikusanya fedha kutoka kwa wanachama wake na wadau mbalimbali, taarifa kutoka chanzo cha kuaminika, zinaeleza sehemu ya fedha hizo zinaishia mifukoni mwa viongozi.
Hayo yamebainika juzi katika kikao cha viongozi wa chama hicho ‘Retreat’ kilichofanyika mkoani Kigoma na kuhusisha wajumbe wote wa Kamati Kuu.
Chanzo hicho kutoka miongoni mwa wajumbe walioshiriki kikao hicho, kinaeleza Mjumbe wa Kamati Kuu, Godbless Lema, ndiye aliyeanza kufichua mambo, baada ya kueleza Heche alipewa mchango wa Shilingi milioni 60 na mdau kwa ajili ya chama hicho, lakini hakuwasilisha hata senti moja.
Mambo yalikwenda mbali zaidi, hadi Lema alipomtaka Heche abishe hadharani kama hakuwahi kupokea kiasi hicho cha fedha. Katika utetezi wake, Heche amedai alidhani fedha hizo anazopewa ni kwa ajili yake binafsi.
Haikuishia hapo, chanzo hicho kinaeleza, kinasema Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu, naye alisema Heche amekula Shilingi milioni 10.
Katika maelezo yake ndani ya kikao hicho, Sugu alisema alimpeleka Heche kukutana na mmoja wa wadau wao kwa ajili ya kupokea mchango wa ujenzi wa chama, cha kushangaza fedha zote hizo hazikufikishwa kwenye chama, zikaishia mifukoni mwa Heche.
Ikumbukwe kuwa, viongozi hao wa Chadema akiwemo Heche, ndiyo wanaosimama majukwaani wakiomba wapewe nafasi ya kuliongoza Taifa kwa ahadi kuwa watasimamia fedha za umma, ilhali usimamizi wa vijisenti vya chama umewashinda.
Huo ni uthibitisho tosha kuwa, Chadema imejaa viongozi wanaofanya kila jambo kwa maslahi yao binafsi, wanajenga kila ushawishi kuwaumiza wananchi ili kujinufaisha na wanatafuta huruma ya umma, ili kukusanya fedha za kunufaisha familia zao.
Mwisho wa kikao hicho, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alimkingia kifua Heche, huku akionya kuwa, vitendo hivyo si vizuri kufanywa na viongozi.
