Mwenyekiti wa Chama cha Mwanasheria wa Serikali, Ado November, amesema tangu Rais Samia Suluhu Hassan ameingia madarakani amesaidia kuimarisha mfumo wa sheria na mabadiliko ya sheria mwaka 2022 yaliyosaidia kuleta mageuzi makubwa nchini.
Amesema kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, Watanzania takribani milioni 8 waliokuwa na kesi mashauri yao yamemalizwa na mawakili wa serikali.
Amesema juhudi hizo za kuimarisha mfumo wa sheria, sera na utawala bora zimeendelea kuzaa matunda, huku zikichochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
Ado ametoa kauli hiyo wakati wa Uzinduzi wa Kitabu cha Falsafa ya Sheria ya Mama Samia uliofanyika leo Julai 10, 2026 katika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM).
Amesema Chama cha Mwanasheria wa Serikali kimeandika na kuhifadhi kumbukumbu za mageuzi yaliyotekelezwa katika Serikali ya Awamu ya Sita, yakilenga kuonesha namna mabadiliko ya kisheria na kisera yalivyoboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, hususan katika sekta ya afya.
Amesema tangu Rais Samia aingie madarakani, Serikali imeweka mkazo katika kufanya mapitio na marekebisho ya sheria mbalimbali ili ziendane na mazingira ya sasa ya maendeleo, mahitaji ya wananchi na mwelekeo wa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo pamoja na mipango mingine ya maendeleo.
Kwa mujibu wa Ado, hatua hizo zimewezesha kuimarika kwa utekelezaji wa sheria, kuongeza ufanisi wa taasisi za umma na kujenga mazingira bora zaidi ya utoaji wa huduma za kijamii na kukuza uchumi wa Taifa.
