Kamati ya Kudhibiti maambukizi ya VVU na UKIMWI (CMAC) ya Halmashauri ya Wilaya ya Magu imewatembelea wavuvi na wafanyabiashara katika mwalo wa Maneto uliopo Kata ya Kahangara wilayani Magu na kuwapa wananchi hao elimu ya kutokomeza maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) pamoja kuwagawia zana za kujikinga na virusi hivyo.
Pia kamati hiyo imewataka wananchi kuandaa mkakati wa ukusanyaji taka katika eneo hilo ili kudhibiti magonjwa ya kuhara kama vile kipindupindu kutokana na msongamano wa watu katika eneo hilo.

Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Diana Philemon ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa baraza la madiwani wa halmashauri hiyo ambapo pamoja na mambo mengine aliwasisitiza wananchi hao kukumbushana kuhusu kupima VVU mara kwa mara ili kuepuka madhara ya ugonjwa wa Ukimwi.
“Tuendelee kujikinga ila pia tuendelee kutumia zana zinazotusaidia kuzuia maambukizi hayo. Kwa wale ambao wamebainika kuwa na maambukizi ni vema kutumia dawa za kufubaza virusi hivyo (ARVs) ili virusi hivyo visiwe na uwezo wa kuenea kwa wengine,” amesema.
Naye Afisa Uvuvi wa Kata ya Kahangara, Musa Kisusi amesema kutokana na elimu ya Ukimwi wanayopewa mara kwa mara, kumekuwa na mwamko wa kutosha kwa wenye VVU kutumia dawa na zana za kujikinga maambukizi ya virusi hivyo.
Aidha, mmoja wa wananchi wanaofanya shughuli za kibiashara katika eneo hilo, Lucas Masanga ameishukuru kamati hiyo kwa kuwapa elimu ya namna ya kujikinga na VVU pamoja na Ukimwi.
“Tunaahidi kuhakikisha Watoto wanaojihusisha na biashara katika eneo hili wanarejea shuleni kuendelea na masomo kwa sababu ni jambo ambalo linakwenda kinyume na taratibu za serikali,” amesema.
