Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amewataka Watanzania kuwa walinzi wa mali za umma, akieleza kuwa mtu anayeharibu miundombinu hiyo, anateketeza kodi za wananchi.
Samia amefafanua kuwa fedha inayokusanywa na Serikali, kisha kutolewa kama mchango katika utekelezaji wa miradi, hizo ni kodi za wananchi, hivyo hawatakubali ziteketezwe kiuhalisi.

Dkt Samia ameeleza hayo leo Agosti 7,2026 wakati akifungua na kutembelea Mradi wa Mabasi Yanayoenda Haraka Awamu ya Pili (BRT II) katika barabara ya Kilwa, Chang’ombe, Sokoine na Kawawa jijini Dar es Salaam.
“Anayefanya hivyo anachelewesha maendeleo ya Taifa, anarudisha nyuma Taifa, analihujumu Taifa, ni adui wa Taifa letu, tusikubaliane nao,” amesema Dkt Samia
Mbali na hilo, Rais Samia amewahisi vijana kutambua kuwa Tanzania ndio nyumbani hakuna kwingine, hivyo wasikubali kutumika bali watunze kila kilichomo nchini.
“Uharibifu wa miundombinu unaibebesha nchi gharama kubwa ya kuirejesha kwa kutumia fedha ambazo zingekwenda kutumika katika miradi mingine. Hakuna faida ya kufanya hivyo, zaidi ya huduma na shughuli za kiuchumi kudhoofika na kasi ya maendeleo ya Taifa kudorora,” amesema Rais Samia.
