You are currently viewing Umeme wa JHPP tayari kusambazwa nchi nzima

Umeme wa JHPP tayari kusambazwa nchi nzima

Wakati Tanzania ikijiandaa kuzindua rasmi Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) Agosti 22, 2026, Serikali imesema maandalizi ya kusafirisha na kusambaza umeme unaozalishwa na bwawa hilo katika maeneo mbalimbali nchini yamekamilika kwa kiwango kikubwa.

Akizungumza katika mahojiano na moja ya vituo vya televisheni mtandaoni, Kamishina wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, amesema njia kuu ya kusafirisha umeme kutoka bwawani hadi Chalinze yenye urefu wa kilomita 160 na msongo wa kilovoti 400 tayari imekamilika.

Luoga amesema njia ya Chalinze hadi Kituo cha Zuzu mkoani Dodoma imefikia asilimia 99 ya utekelezaji na inatarajiwa kukamilika mwezi huu, ikiwa ndiyo itakayobeba umeme wote kutoka mitambo tisa ya JNHPP.

Amesema kutoka Zuzu, umeme huo utasambazwa katika mikoa ya Iringa, Mbeya, Rukwa, Tabora, Shinyanga, Mwanza, Singida na Arusha, huku ukiunganishwa pia na gridi za Zambia na Kenya.

Kwa mujibu wa Luoga, kukamilika kwa miundombinu hiyo kutaruhusu mitambo yote tisa ya JNHPP kufanya kazi kwa uwezo wake kamili, hatua inayotarajiwa kuimarisha upatikanaji wa umeme na kuchochea shughuli za uzalishaji nchini.