Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga amembana Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, John Heche kwa maswali magumu kutoka upande wa Jamhuri katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Antipas Lissu.
Wakili Katuga amemuhoji Heche kuhusu mali, magari na miamala ya fedha kwenye akaunti yake binafsi.
Katika hatua hiyo ya ushahidi, Katuga alimuuliza Heche kuhusu chanzo cha mapato yake pamoja na hali yake ya kifedha. Heche alieleza Mahakama kuwa halipwi mshahara wala posho na CHADEMA kutokana na nafasi yake ya Makamu Mwenyekiti.
Hata hivyo, wakati akiendelea kuhojiwa kuhusu mali anazomiliki, nyaraka za umiliki wa magari ziliwasilishwa mbele ya Majaji. Heche alikiri kumiliki au kutumia magari kadhaa, yakiwemo Mitsubishi Canter, Toyota Crown, Hilux Double Cabin na Prado, pamoja na trekta.
Hoja nyingine iliyoibua maswali mahakamani ilihusu miamala ya fedha kwenye akaunti ya Heche katika benki ya CRDB.
Katuga alimuuliza Heche kuhusu mtu aliyetajwa kwa jina la Salman Nilesh. Heche alieleza kuwa hamfahamu mtu huyo. Hata hivyo, risiti ya CRDB iliyowasilishwa mahakamani ilionyesha kuwa Sh milioni 20 ziliingizwa kwenye akaunti ya Heche tarehe 11 Novemba 2024, huku jina la Salman Nilesh likitajwa kwenye muamala huo.
Heche alikiri mbele ya Mahakama kuwa akaunti hiyo ni yake na kwamba fedha hizo ziliingia kwenye akaunti hiyo.
Jamhuri iliwasilisha pia risiti nyingine ya CRDB ya Oktoba 17, 2024, inayoonyesha kuwa kiasi cha Sh milioni 10 kiliingizwa kwenye akaunti hiyo hiyo, huku jina la Salman Nilesh likitajwa tena.
Kwa mujibu wa nyaraka hizo zilizowasilishwa mahakamani, miamala hiyo miwili ilifikisha jumla ya Sh milioni 30 ndani ya kipindi cha takribani mwezi mmoja.
Hoja hiyo imeibua swali mahakamani kuhusu uhusiano kati ya Heche na mtu huyo pamoja na chanzo na madhumuni ya fedha hizo, huku maswali na majibu ya shahidi yakiendelea kuwa sehemu ya mchakato wa kesi.
